Join Our Groups
TOPIC 2: UENEAJI WA KISWAHILI
ENZI ZA WAINGEREZA NA BAADA YA UHURU
Ukuaji na Ueneaji wa
Kiswahili katika enzi ya Waingereza
Waingereza
walipochukua koloni la Tanganyika kutoka kwa Wajerumani walikuta Kiswahili
kimeimarika na kinatumika katika maeneo mengi ya nchi. Kwa kuwa nao walihitaji
kutawala hawakupuuzia matumizi ya Kiswahili katika utawala wao japo hawakutumia
Kiswahili kwa lengo la kukikuza lakini walijikuta wanakieneza na kukikuza bila
ya wao kukusudia.
Mambo waliyochangia Waingereza katika Ukuaji wa Kiswahili nchini Tanzania
Waingereza walitumia Kiswahili kama nyenzo ya kusaidia shughuli zao za kiutawala. Hata hivyo kuna mambo waliyofanya waingereza yaliyosaidia kukua na kuenea kwa Kiswahili, mambo hayo ni kama yafuatayo:
1. Shuguli za
Kiuchumi
Shuguli
za kiuchumi wakati wa Waingereza zilihusisha kilimo na biashara. Kwa upande wa
klimo, Waingereza waliendesha kilimo cha mazao mbalimbali, na walitumia mfumo
wa kuajiri vibarua kutoka sehemu mbalimbali za nchi. Vibarua hao walijulikana
kwa jina la manamba.
Katika
mkusanyiko wa vibarua hawa waliokuwa na usuli wa makabila tofautitofauti, lugha
pekee iliyoweza kuwaunganisha ni Kiswahili ikizingatiwa kwamba Kiswahili
kiliteuliwa kuwa lugha rasimi katika mawasiliano ya kiutawala. Walilazimika kuzungumza
Kiswahili kwani bila hivyo mawasiliano yasingeweza kufanyika kwa urahisi.
Hata
hivyo kupitia shuguli za kilimo maneno mapya ya Kiswahili yaliweza kuzaliwa,
kwa mfano: yadi, belo, belingi, bani, mtama n.k, kwa hiyo kupitia shughuli hizi
Kiswahili kilizidi kukua.
2. Shuguli za Kiutamaduni
Shughuli
hizi ni kama vile uigizaji wa tamthiliya za kigeni, uchezaji wa mziki wa kigeni
hususani twisti. Tamthiliya za kigeni zilikuwa zikiigizwa majukwaani kwa lugha
ya Kiswahili na hivyo ikasaidia kukua kwa msamiati wa Kiswahili.
3. Shughuli za Kidini
Wakati
wa utawala wa mwingereza pia kuliambatana na ujio wa wamishonari waliokuwa na
lengo la kueneza dini ya kikristo. Katika harakati hizi walitumia lugha ya
Kiswahili ili kufanikisha malengo yao ikizingatiwa kwamba Kiswahili kilikuwa
kimeshaenea vya kutosha wakati wa utawala wa Mjerumani, kwa hiyo wamishonari wa
Kiingereza waliendelea kukiimarisha zaidi.
Pia
shughuli za kidini zilipelekea kutafsiriwa kwa vitabu mbalimbali vya kidini
kama vile Biblia na vitabu vingine. Tafsiri ya vitabu hivi ilikuwa ni kutoka
katika lugha ya kiingereza kwenda katika lugha ya Kiswahili. kwa kufanya hivi
Kiswahili kiliweza kuingiza msamiati mwingi sana na hivyo kukuza lugha ya
Kiswahili.
Wamishonari
walilazimika kujifunza Kiswahili hukohuko kwao ili wanapokuja huku Afrika
Mashariki wasipate tabu ya kujifunza Kiswahili. Kwa sababu hii wamishonari
waliokuwa wamekwishajifunza lugha ya Kiswahili walitunga kamusi za Kiswahili –
Kiingereza ili kuwasaidia wenzao pia kujifunza Kiswahili; kwa njia hii waliweza
kukikuza Kiswahili.
4. Shughuli za
kisiasa
Shughuli
za kisiasa hasa katika uanzishwaji wa vyombo mbalimbali vya kiutawala, jeshi,
polisi, mahakama, boma n.k. Kufuatia uanzishwaji wa vyombo hivi msamiati mwingi
wa Kiswahili uliweza kuzuka na hivyo kukuza Kiswahili.
5. Shughuli za
kiutawala
Makampuni
ya uchapishaji yalianzishwa (East African literature Bureau), na kamati ya
lugha iliundwa (Interterritorian language committee). Hatua hii iliimarisha
matumizi ya lugha ya Kiswahili hali iliyosaidia kukua kwa lugha ya Kiswahili.
6.
Shuguli za
ujenzi wa reli na barabara
Shughuli
hizi pia zilisaidia kuibuka kwa msamiati mpya kama vile, reli, stesheni,
tiketi n.k.
7. Usanifishaji
wa Kiswahili
Usanifishaji
wa lugha ya Kiswahili pia lilikua ni jambo jingine muhimu sana lililosaidia
kukua kwa msamiati wa Kiswahili. Lengo la usanifishaji wa Kiswahili lilikuwa ni
kuleta ulinganifu wa matumizi ya lugha ya Kiswahili katika ukanda wa Afrika
Mashariki.
UENEAJI WA KISWAHILI
Ukuaji
na Ueneaji ni maneno mawili yenye maana zinazokaribiana lakini
zinazotofautiana. Ukuaji humaanisha ongezeko la msamiati katika lugha na
ueneaji ni uongezekaji wa matumizi ya lugha kieneo. Kwa hiyo hapa tutaangalia
yale mambo yaliyosababisha Kiswahili kitumike katika eneo kubwa. Mambo hayo ni
haya yafuatayo:
1.
Vyombo vya
habari
Vyombo
vya habari vilivyokuwepo kwa wakati huo ni redio, magazeti na majarida
mbalimbali. Kwa upande wa redio kulikuwepo na redio Tanganyika iliyoanza
kurusha matangazo yake kwa kutumia lugha ya Kiswahili. Na magazeti yaliyokuwa
yakichapishwa wakati huo ni pamoja na: Mambo leo, Sauti ya Pwani, Kiongozi na
Habari za leo. Magazeti haya yote yalikuwa yakichapishwa kwa lugha ya
Kiswahili. Kwa hiyo kwa kutumia vyombo vya habari (redio na magazeti) kiswahili
kiliweza kuenea.
2.
Kilimo
Kupitia
kilimo watu waliweza kukutana pamoja, watu wa makabila tofautitofauti. Kwa hiyo
katika kipindi chote walichokaa kwenye makambi ya mashambani waliweza kujifunza
Kiswahili na walipomaliza muda wao walirudi nyumbani wakiwa wamejifunza lugha
mpya na hivo kwa njia hii waliweza kuieneza lugha ya Kiswahili.
3.
Muundo wa
jeshi la kikoloni (KAR)
Jeshi
la KAR liliundwa na watu kutoka makabila mablimbali, na lugha iliyokuwa
ikitumika jeshini ni Kiswahili, askari hawa walisaidia kueneza lugha ya
Kiswahili ndani na nje ya nchi kwani kila walipokwenda walikuwa wakizungumza
Kiswahili.
4.
Mfumo wa
elimu
Chini
ya utawala wa Waingereza Kiswahili kilitumika katika masomo yote kwa ngazi ya
shule ya msingi, na pia kilitumika kama somo kwa ngazi ya shule za sekondari.
Kwa hiyo hii pia ilichangia kuenea kwa lugha ya Kiswahili
5.
Harakati za
kudai uhuru
Chama
cha TANU kilianzisha harakati za kudai uhuru, harakati hizo ziliendeshwa kwa
lugha ya Kiswahili. Kwa hiyo kupitia harakati hizo Kiswahili kiliweza kuenea
kwa kiwango kikubwa.
Tathimini ya Maendeleo
ya Kiswahili wakati wa Waingereza
Licha
ya maendeleo ya lugha ya Kiswahili katika utawala wa Waingereza, pia kulikuwa
na changamoto zilizoikabili lugha ya Kiswahili katika kupiga hatua ya
maendeleo. Changamoto hizo ni kama zifuatazo:
1.
Kutofundishwa kwa Kiswahili shule zote nchini
Wakati
wa utawala wa Waingereza Kiswahili kilifundishwa katika shule za watoto wa
kiafrika tu, wakati katika shule za watoto wa kizungu Kiswahili
hakikufundishwa. Kwa hiyo suala hili lilifanya Kiswahili kipewe msukumo mdogo
sana na hivyo kuhafifisha ukuaji wake.
2.
Kutotumika kwa Kiswahili kama lugha ya kufundishia
Lugha
ya Kiswahili ilitumika kufundishia katika shule za msingi pekee ilihali lugha
ya kiingereza ilitumika kuanzia shule za sekondari hadi elimu ya juu. Hali hii
ilisababisha watu kujitahidi sana kujifunza kiingereza; kwa kuzungumza
kiingereza ilikuwa na ishara kwamba wewe ni msomi, na hivyo kutokana na hali
hii Kiswahili kilendelea kukua polepole sana.
3.
Kukosekana kwa vyombo vya kizalendo vya kukuza Kiswahili
Vyombo
vilivyokuwa vinahusika na masuala ya ukuzaji wa Kiswahili wakati wa ukoloni vilikuwa
vimeanzishwa na wakoloni wenyewe, kwa mfano Kamati ya Lugha ya Afrika Mashariki
(Inter-Territorial Swahili Language commitee) na Shirika la maandiko la Afrika
Mashariki (East African Literature Bureau). Katika hali kama hii ukuzaji wa
Kiswahili ulikosa msukumo mkubwa wa kizalendo.
4.
Kasumba ya kuthamini Kiingereza
Wananchi
walikuwa na kasumba kwamba mtu anayezungumza Kiingereza alichukuliwa kuwa ni
mtu mwenye maendeleo na msomi, kwa hiyo hali hii ikapelekea watu kutothamini
Kiswahili na hivyo Kiswahili kudharaulika.
UKUAJI NA UENEAJI WA
KISWAHILI BAADA YA UHURU
Baada
ya uhuru kuna harakati mbalimbali zilizochukuliwa na serikali ya Tanzania
katika kukiendeleza na kukikuza kiswahili. Harakati hizo ni pamoja na
kupendekezwa
kuwa lugha rasmi 1962. Mkwaka 1964 kiswahili kilipendekezwa kuwa lugha ya taifa
na kuwa kitatumika katika shughuli zote za kiserikali na kitaifa mfano katika
elimu hususani elimu ya msingi.
Kuundwa
kwa Chombo cha usanifishaji ambacho kilikuwa na kazi ya kuhimiza maendeleo ya
kiswahili, kutayarisha kamusi na vitabu mbalimbali vya sarufi na fasihi ya
lugha ya kiswahili na kuandaa wataalamu watakaoshughulikia usanifishaji wa
Kiswahili
Pia
baada ya uhuru kulianzishwa Taasisi mbalimbali zitakazoshughulikia lugha ya
kiswahili. Mfano:- BAKITA, TUKI, TUMI, UKUTA, UWAVITA, Idara ya Chuo Kikuu Cha
Dar es Salaamu.
Shughuli mbalimbali zinazowezesha Kukua na Kuenea kwa Kiswahili nchini
Baada
ya uhuru nchini Tanzania kiswahili kilienea kwa kasi kubwa sana. Kuna sababu
mbalimbali ambazo zilichangia kukua na kuenea kwa kiswahili hapa nchini. Baadhi
ya sababu hizo ni pamoja na kuteuliwa kwa kiswahili kuwa lugha ya Taifa,
Kiswahili kitumike katika Elimu, mfano kuwa lugha ya kufundishia katika shule
za msingi. Kuundwa kwa vyombo mbalimbali vya kukuza na kuneza kiswahili,
Kiswahili kuwa Lugha rasmi na lugha ya Taifa, shughuli mbalimbali za kidini,
shughuli za kisiasa na kiutawala na shughuli za kiutamaduni na uchapishaji wa
vitabu na majarida mbalimbali.
1.
Kiswahili kuwa lugha ya taifa
Baada
ya uhuru mwaka 1962 kamati iliundwa ili kuangalia uwezekano wa kutumia
kiswahili katika shughuli zote rasmi, mfano bungeni na shughuli zote za
kiofisi. Pia kiswahili kiliteuliwa kuwa lugha ya taifa 1964 ambapo katika
shughuli zote za kitaifa zitaendeshwa kwa kutumia lugha ya kiswahili. Hivyo
kiswahili kilihimizwa kutumika katika mawasiliano yote hasa katika shughuli za
umma na Wizara zote, Serikali na Bunge, kiswahili kiliendelea kupanda hadhi zaidi
wakati wa Azimio la Arusha la mwaka 1967 kwani azimio hilo lilitungwa na
kuandikwa kwa lugha ya kiswahili.
2.
Kuundwa kwa vyombo vya ukuzaji na uenezaji wa Kiswahili
Tanzania
baada ya uhuru ilifanya jitihada za kuunda vyombo mbalimbali vya kukuza na kueneza
Kiswahili katika nyanja mbalimbali mfano wa vyombo hivyo ni UWAVITA BAKITA,
TUKI, Taasisi ya Elimu, TAKILUKI na Chama cha Kiswahili Chuo Kikuu Dar es
Salaam.
3.
Kutumika katika elimu
Kiswahili
licha ya kutumika katika shughuli mbalimbali za kiserikali, kilipendekezwa
kutumika katika shule za Msingi na kufundishwa katika elimu ya sekondari kama
somo na katika vyuo vikuu wanatoa shahada mbalimbali za lugha ya kiswahili. Pia
katika Elimu ya watu wazima ambao hawakujua kusoma na kuandika. Watu hawa walijifunza
masomo mbalimbali kwa lugha ya kiswahili na kuwafanya watu wengi kujua kusoma,
kuandika na kuzungumza lugha ya kiswahili fasaha. Kampeni hii ilikuwa kwa nchi
nzima ambapo walijifunza elimu ya Afya, Siasa, Kiswahili, Kilimo na ufundi kwa
lugha ya Kiswahili na kuwafanya watu wengi kuzungumza kiswahili sanifu.
4.
Vyombo vya habari
Tangu
uhuru ulipopatikana kuna vyombo mbalimbali vya habari vilivyoanzishwa. Vyombo
hivi hutumika kueneza kiswahili kwa kiasi kikubwa na hufikiwa na watu wengi
licha ya kuwepo kwa changamoto za kiuchumi. Vyombo hivyo ni magazeti na
majarida mbalimbali ambayo huandikwa kwa lugha ya kiswahili lakini kuna redio
na runinga ambazo matangazo yake hutangazwa kwa lugha ya kiswahili. Hivyo
kukifanya kiswahili kuenea kote ndani na nje ya nchi.
5.
Biashara
Shughuli
za kibiashara nchini husaidia kuenea na kukua kwa kiswahili kutokana na kuwepo
kwa makabila tofauti tofauti ambapo wafanyabiashara huweza kuunganishwa kwa
lugha ya kiswahili. Hivyo kiswahili hudumishwa na kutumika katika biashara
hizo.
6.
Shughuli za siasa na utawala
Tangu
wakati wa harakati za kupigania uhuru kiswahili kimetumika kama nyenzo muhimu
kuwaunganisha wananchi. Shughuli za kisiasa zimetumia lugha hii katika
kujiimarisha; mfano wakati wa chama kimoja, Azimio la Arusha na Mfumo wa vyama
vingi Kiswahili kimetumika kama njia kuu ya mawasiliano. Pia katika utawala
chama kinachotawala kimekuwa na harakati za kukiendeleza kiswahilli katika
nyanja zote. Ambapo kiswahili kimekuwa kikitumika katika shughuli zote za
kiutawala. Hivyo shughuli za kisiasa na kiutawala zimechangia kwa kiasi kikubwa
katika kukuza, kukieneza na kukiendeleza kiswahili.
7.
Uandishi na uchapishaji wa vitabu
Kuibuka
kwa waandishi wa vitabu mbalimbali vya kiswahili vya sarufi na fasihi ambavyo
vilichambua kwa kina mambo mabalimbali yahusuyo lugha ya kiswahili na utamaduni
wake, mfano :- F Nkwera, Shabani Robart, Mathias Mnyapala na Shaffi Adam
Shaffi. Waandishi wengine chipukizi walijitokeza na wanaendelea kujitokeza
katika tasnia hii ya uandishi wa vitabu.
8.
Shughuli za kiutamaduni
Shughuli
za kiutamaduni zimechangia kueneza kukuza na kuendeleza lugha ya Kiswahili.
Shughuli hizo ni pamoja na harusi, misiba, matanga na sherehe mbalimbali za
kijamii ambazo zimesaidia kukiendeleza Kiswahili kwa kuwa huwakutanisha watu
tofautitofauti katika shughuli hizo, ambapo huwalazimu kutumia lugha ya
kiswahili katika mawasiliano na kufanya kiswahili kuendelea. Pia katika Sherehe
mbalimbali vikundi vya sanaa na muziki vinavyotumia lugha ya kiswahili
kutumbuiza. Vikundi vingine huandaa nyimbo zao kwa ajili ya kukieneza
Kiswahili.
VYOMBO VYA UKUZAJI NA
UENEZAJI WA LUGHA YA KISWAHILI
Tangu
Tanzania ipate uhuru hadi sasa kuna vyombo kadha wa kadha vilivyoanzishwa kwa
ajili ya kukuza na kueneza Kiswahili baadhi ya vyombo hivyo ni hivi vifuatavyo:
BAKITA
Hii
ni taasisi ya serikali iliyoundwa kwa sheria ya Bunge Na.27 ya mwaka 1967 kwa
madhumuni ya kukuza Kiswahili. Kutokana na sheria hii Baraza ndilo mratibu wa
kusimamia asasi zote na mawakala wote wanaokuza Kiswahili katika Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania.
BAKITA
imekuwa na mchango mkubwa sana katika ukuzaji na uenezaji wa lugha ya Kiswahili
kupitia majukumu yake. Majukumu ya Baraza kama yalivyofafanuliwa katika sheria
hiyo ni haya yafuatayo:
1. Kuratibu na kusimamia maendeleo na matumizi ya
Kiswahili nchini kote.
Katika kufanya hivi Baraza lina jukumu la kuhakikisha Kiswahili kinaendelea na
kuhakikisha kuwa matumizi ya Kiswahili yanakuwa sahihi.
2. Kushirikiana na vyombo vingine nchini
vinavyojihusisha na maendeleo ya Kiswahili na kuratibu shughuli zao. Vyama vya Kiswahili kama vile
CHAKAMA, CHAWAKAMA vina mchango mkubwa wa kukuza na kueneza lugha ya Kiswahili
kwa kushirikiana na BAKITA. Ushirikiano wa BAKITA na vyama hivi waweza kuwa ni
wa kuto ushauri, au msaada wa kifedha, kwa mfano BAKITA imekuwa ikiwasaidia
CHAWAKAMA pale wanapokuwa wanataka kufanya makongamano nap engine wanahitaji
msaada wa kifedha, kwa hiyo BAKITA imekuwa ikiwasaidia kifedha.
3. Kuhimiza matumizi ya Kiswahili katika shughuli
rasmi na za kawaida.
BAKITA imekuwa ikiandaa vipindi mbalimbli redioni ili kuhimiza matumizi sahihi
ya lugha ya Kiswahili.
4. Kushirikiana na mamlaka zinazohusika kuthibitisha
tafsiri sanifu za istilahi.
Katiaka uundaji wa istilahi, BAKITA imekuwa ikichapisha vitabu mbalimbali
ikionesha istilahi sanifu zilizoingizwa katika lugha ya Kiswahili. kwa hiyo
kupitia jukumu hili Kiswahili kimekuwa kinakua.
5. Kutoa huduma za tafsiri na ukalimani kwa
serikali, mashirika ya serikali na yasiyo yaserikali na asasi nyingine. Kupitia tafsiri zinazofanywa na
BAKITA Kiswahili kimekuwa kikikuwa na kuenea.
6. Kuchapisha jarida au toleo linalohusu lugha na
fasihi ya Kiswahili.
Machapisho haya ya BAKITA yanaendelea kukifanya Kiswahili kukua kwa kuongeza
msamiati mpya na hivyo watu wanaposoma machapisho hayo wanajifunza msamiati
mpya na hivyo kufanya Kiswahili kukua.
7.
Kushirikiana na mashirika ya kitaifa, asasi na watu binafsi, kufuatilia,
kushauri na kusimamia shughuli zinazolenga kukuza Kiswahili nchini Tanzania.
8. Kutoa ushauri kwa waandishi na wachapishaji ili
watumie Kiswahili fasaha.
Kwa kufanya hivi matumizi bora ya Kiswahili yanakuwa yanaimarika.
9. Kushirikiana na Wizara ya Elimu na Mafunzo ya
Ufundi kuthibitisha vitabu vya Kiswahili vitakavyotumika shuleni na
vyuoni kabla havijachapishwa.
Hili pia ni jamabo linaloimarisha matumizi ya Kiswahili sanifu.
TAKILUKI
Taasisi
ya Kiswahili na Lugha za Kigeni (TAKILUKI) ilianzishwa mwaka 1979 kwa lengo la
kukuza na kueneza lugha ya Kiswahili ndani na nje ya Zanzibar, ili kutimiza
lengo hilo TAKILUKI inajishughulisha na kazi zifuatazo:
1.
Kuratibu na kuendesha mafunzo ya lugha ya Kiswahili visiwani Zanzibar,
kuendesha mafunzo ya lugha ya Kiswahili kwa wazawa na wageni, kuhariri miswada
mbalimbali ili kuthibitisha ufasaha wa Kiswahili na kufanya tafiti za Kiswahili
katika Nyanja zake zote, hususani katika uwanja wa sarufi na fasihi.
2.
Pia TAKILUKI wana kazi ya kuandaa istilahi za taaluma mbalimbali, kutoa huduma
za taaluma mbalimbali, kutoa huduma za tafsiri na ukalimani kwa lugha
mabalimbali kwa mashirika, idara, wizara, taasisi, kampuni na watu binafsi,
kufundisha lugha za kigeni na kuandika vitabu mbalimbali vya Kiswahili.
3.
Pia hujishughulisha na utoaji wa ushauri wa kitaaluma kwa watunzi wa vitabu ili
waweze kuandika kazi zenye ubora, na kushirikiana na wadau wengine wa Kiswahili
kama vile, mashirika, wizara, taasisi, vyuo na watu binafsi katika kuendesha
shuguli za ukuzaji wa Kiswahili, mathalani kuandaa na kuendesha semina, warsha
na kozi fupifupi za Kiswahili.
4.
Vilevile hujishugulisha na usimamizi na ufuatiliaji wa matumizi sahihi ya lugha
ya Kiswahili katika vyombo vya habari na katika shughuli mbalimbali za serikali
na za kawaida.
TUKI/TATAKI
Majukumu
ya TUKI ni pamoja na kuunda sera muafaka za kustawisha Kiswahili na pia kufanya
utafiti katika lugha ya Kiswahili. Majukumu mengine ya TUKI ni kuhariri,
kuchapisha vitabu na kutawanya vitabu na majarida ya kitaaluma katika Kiswahili.
Kwa sasa TATAKI inatoa shahada ya awali na uzamili katika lugha ya Kiswahili,
kwa njia hii inawaandaa wataalamu wa lugha ya Kiswahili ambao watatumika sehemu
mbalimbali za ulimwengu kufundisha lugha ya Kiswahili.
CHAUKIDU
CHAUKIDU
ni kifupi cha Chama cha Ukuzaji wa Kiswahili Duniani, makao makuu ya chama hiki
kwa sasa yapo chuo kikuu cha Wisconsin-Madison, Marekani
Madhumuni Makuu ya
CHAUKIDU ni:
Kuwajumuisha
pamoja wakuzaji wa Kiswahili duniani kote kwa lengo la kuchochea kasi ya malengo
mahususi yafuatayo:
1. Kukuza Kiswahili katika nyanja zote ambamo lugha hii
inatumika au inaweza kutumika na kuongeza ufanisi wa mawasiliano katika
ufundishaji na utafiti wa maarifa ya aina zote, uandishi/utangazaji wa habari,
uandishi wa vitabu, uchapishaji vitabu na majarida, utayarishaji wa safari za
mafunzo katika Afrika ya Mashariki na Kati, n.k.
2. Kusambaza habari na matokeo ya utafiti kwa kutumia machapisho mbalimbali
na teknolojia ya mtandao wa kompyuta juu ya vipengele mbalimbali vya Kiswahili
na masuala yanayohusiana na Kiswahili.
3. Kuwajumuisha wanachama kwa ajili ya kubadilishana mawazo
na tajiriba zao katika masuala mbalimbali yanayohusu Kiswahili (k.v. uboreshaji
wa ufundishaji, utangazaji, utafiti, uandishi, nk.) kwa njia ya mkutano wa kila
mwaka, warsha au semina au kongamano maalumu, na hata kwa njia ya mtandao.
4. Kuelimisha umma juu ya umuhimu wa kujivunia,
kuendeleza, na kuheshimu Kiswahili.
5. Kushauri ama kushinikiza serikali za nchi ambamo Kiswahili
kinazungumzwa kutambua thamani iliyobebwa na maliasili hii ili kuunda sera
muafaka za kukiendeleza kadri ya uwezo wake kwa manufaa ya maendeleo ya
serikali na watu wake kijamii, kisiasa, kiuchumi, kiutamaduni, kielimu, n.k.
CHAWAKAMA
CHAWAKAMA
husimama badala ya Chama cha Wanafunzi wa Kiswahili vyuo vikuu Afrika
Mashariki. Chama hiki kilianzishwa mwaka 2004 kwa lengo la kukuza na kueneza
Kiswahili katika eneo lote la Afrika Mashariki kupitia wanafunzi wanaosoma
Kiswahili vyuoni. Wanachama wa chama hiki ni wale wanosoma Kiswahili na hata
wale wenye mapenzi ya lugha ya Kiswahili pia wanaweza kujiunga na chama hiki.
Chama
hiki kina utaratibu wa kuandaa makongamano ambapo wanachama wake kutoka nchi
zote za Afrika Mashariki hupata fursa ya kukutana mara moja kila mwaka. Pamoja
na utaratibu wa chama kuandaa makongamano pia uanzishwaji wake umeambatana na
malengo kadhaa ambayo ndiyo dira inayoiongoza chama kwa mujibu wa katiba,
malengo hayo ni haya yafuatayo:
1.
Kuwapa wanachama nafasi ya kujadili, kuimarisha, kuendeleza na kukuza vipawa
vyao vya lugha na fasihi ya Kiswahili.
2.
Kuamsha ari ya mapinduzi ya utamaduni wa lugha ya kiswahili.
3.
Kueneza lugha ya kiswahili ndani na nje ya nchi.
4.
Kushirikiana na vyama vingine katika juhudi za kuendeleza na kuimarisha lugha
ya kiswahili ndani na nje ya nchi wanachama.
5.
Kuwaunganisha wanafunzi wa kiswahili Afrika Mashariki na kati katika kukikuza
kiswahili.
6.
Kushirikiana na asasi mbalimbali zinazojihusisha na ukuzaji na uenezaji wa
kiswahili ndani na nje ya nchi kama vile BAKITA, TATAKI, TAKILUKI, UWAVITA,
CHAKAMA, BAKIZA n.k.
7.
Kuchapisha kijarida cha chama na machapisho mengine ili kusaidia kueneza
taaluma ya kiswahili.
8.
Kuweka kumbukumbu ya wataalamu wa kiswahili kwa nia ya kuwatumia katika
kufanikisha malengo ya chama na wadau wa Kiswahili.
9.
Kuratibu makongamano na mijadala mbalimbali inayohusiana na taaluma ya
kiswahili.
Pamoja
na malengo hayo, lengo kuu la chama hiki ni kueneza Kiswahili lakini sasa
wanakienezaje? Wanachama wa chama hiki ambao ni nchi wanachama wa jumuia ya
Afrika mashariki wanakawaida ya kuandaa makongamano kwa ngazi ya kitaifa na
ngazi ya kimataifa.
Kwa
ngazi ya kitaifa kila nchi huandaa kongamano kila mwaka ambalo linawakutanisha
wanachama wote kutoka vyuo mbalimbali katika nchi husika. Katika kongamano hilo
mada mbalimbali zinazohusu lugha ya Kiswahili na mustakabali wake hujadiliwa
lakini pia maazimio mbalimbali huchukuliwa juu ya maendeleo ya chama.
Kamusi ya Kiswahili |
DHIMA YA KILA ASASI INAYOKUZA KISWAHILI
Mafanikio
na Changamoto Zinazovikabili Vyombo vya Ukuzaji wa Kiswahili
Mafanikio
Vyombo
vya ukuzaji wa Kiswahili vimejitahidi sana kukuza lugha ya Kiswahili, kwa hali
ya Kiswahili ilivyo sasa ni matokeo ya juhudi za vyombo hivyo. Mafanikio ya
vyombo hivyo ni pamoja na haya yafuatayo:
1.
Machapisho ya lugha ya Kiswahili ni mengi sana nchini na nje ya nchi, kufanya
mafunzo ya Kiswahili, kukua kwa matumizi ya Kiswahili na kuongezeka kwa idadi
ya watumiaji wa Kiswahili nchini.
2.
Matumizi ya lugha ya Kiswahili katika sehemu rasmi hasa katika ofisi za
serikali na ofisi za watu binafsi inadhihirisha mafanikio ya jitihada za vyombo
hivi kuhimiza matumizi ya lugha ya Kiswahili.
3.
Kufundshwa kwa lugha ya Kiswahili kama taaluma kwa ngazi ya shahada ya awali,
uzamili na uzamivu. Hizi ni jitihada za TATAKI katika kuhakikisha kunapatikana
wataalamu wa lugha ya Kiswahili, hivi sasa TATAKI wanafundisha lugha ya
Kiswahili kwa ngazi ya shahada ya awali, uzamili na uzamivu.
4.
Matumizi ya lugha ya Kiswahili katika vyombo mabalimbali vya kimataifa,
matumizi ya lugha ya Kiswahili katika vikao vya Umoja wa Afrika na pia
ufundishwaji wa lugha ya Kiswahili katika vyo mabalimbali Duniani ni ishara
tosha ya kuonesha mafanikio ya jitihada za vyombo vya ukuzaji na uenezaji wa
Kiswahili.
Changamoto
1.
Vyombo hivi vinakabiliwa na upungufu wa wataalam. Wataalamu wengi waliobobea
katika taaluma za Kiswahili wanakimbilia nje ya nchi wakidhani huko ndiko kuna
maslahi mazuri zaidi.
2.
Upungufu wa fedha za kuendeshea shughuli za ukuzaji wa Kiswahili katika vyombo
hivi pia limekuwa ni tatizo sugu. Kwa hiyo shughuli za ukuzaji wa Kiswahili
zinakuwa zinakwenda taratibu.
3.
Taasisi hizi pia zinashindwa kujitangaza vizuri kutokana na kwamba hazina
vyombo vya habari binafsi ambavyo vingeweza kutumika kutangaza shughuli zao.
Jambo hili limesababisha vyombo hivi kushindwa kutoa elimu ya Kiswahili kwa
kutumia vyombo vya habari kutokana na kwamba gharama za kufanya hivyo ni kubwa.
4.
Vyombo hivi baadhi havina ofisi za kudumu, na hivyo kuhamahama jambo ambalo
linaathiri utendaji kazi wa vyombo hivyo.
Naingiaje nianze kupata notes na maswali?
ReplyDeleteNimependa sana somo lakini maswali tutayapataje???? Hili kujipima
ReplyDelete