Join Our Groups
TOPIC 5: UANDISHI
UANDISHI WA INSHA ZA
KIADA
Insha
ni kifungu cha maandishi kilichoandikwa kutokana na mtazamo wa mwandishi katika
kujadili juu ya mada fulani. Mwandishi anaweza kuandika kuipinga mada hiyo au
kuishadidia mada hiyo. Kuna aina mbili za insha, insha za kaida (zisizo za
kisanaa) na insha za kisanaa.
Insha za kaida ni
insha zinazotumia lugha ya kawaida kuelezea mambo mbalimbali katika jamii,
mfano juu ya mazingira, uchumi, biashara, historia n.k.
Muundo wa Insha za
Kaida
1. Kichwa cha insha; kichwa cha insha hudokeza kile
ulichokijadili katika insha yako. Kwa mfano: Madhara ya matumizi ya madawa ya
kulevya n.k
2. Utangulizi; Mambo yaliyopo katika utangulizi
ni pamoja na kutoa fasili ya maneno muhimu na kuelezea kwa muhtasari mambo ambayo
utakwenda kuyajadili katika insha yako.
3. Kiini
cha insha;
katika kiini ndipo kuna maelezo ya kina juu ya kile unachokijadili katika insha
yako, maelezo haya yanakuwa katika aya kadhaa kulingana na idadi ya hoja
ulizonazo katika mjadala wako.
4. Hitimisho; hapa ndipo kuna muhtasari wa kile
kilichojadiliwa katika kiini cha insha au inaweza kuwa ni msimamo juu ya kile
kilichohadiliwa katika insha.
Mambo ya Kuzingatia
katika Uandishi wa Insha
Taratibu
za uandishi zinapozingatiwa insha pia itasomeka vizuri na pia itakuwa na
mtiririko mzuri wa mawazo.
1. Epuka kutumia vifupisho vya maneno visivyo rasmi.
Uandishi wa insha ni suala rasmi,
kwa hiyo katika uandishi wake inatakiwa kuzingatia kuepuka kutumia vifupisho
ambavyo sio majumui yaani havijulikani. Kwa mfano maandishi kama, xamahani
(samahani), ckatai (sikatai) na mengine yafananayo kama hayo ni lazima yaepukwe
katika uandishi wa insha.
2. Andika utangulizi unaovuta umakini wa msomaji.
Hiki ni
kipangele cha muhimu sana, msomaji anapoona kwamba kwenye utangulizi hakuna
kitu kinachomvutia hataendelea kuhangaika kusoma insha hiyo.
3. Andika kiini cha insha kwa mpangilio mzuri.
Unatakiwa
kuandika insha yako katika mpangilio mzuri huku kila wazo kuu likipewa aya yake
na kuwepo na mtiririko mzuri wa mawazo.
4. Andika hitimisho la insha likiwa linahitimisha
mawazo yaliyokwishajadiliwa katika kiini. Hakikisha unapofanya hitimisho epuka
kudokeza wazo jipya ambalo linazua mjadala mpya, hakikisha hitimisho lako
linabeba mawazo uliyokwisha yajadili katika insha yako na wala yasiwe mawazo
yanayotoka nje ya kile ulichokijadili.
Kuandika Insha |
UANDISHI WA HOTUBA
Hotuba
ni insha ambayo hutoa maneno halisi ya mzungumzaji/kiongozi anapozungumzia
hadhira, kuhusu jambo fulani. Insha ya hotuba huandikwa katika hali ya usemi
halisi na mwandishi hatakiwi kuweka alama za kunukuu anapoanza insha yake. Hotuba
inaweza kutolewa na kiongozi wa kisiasa, utawala, kidini, kikundi, shirika
fulani, daktari, n.k. Hadhira katika hotuba husheheni wageni waalikwa,
wanachama, wafuasi, wananchi, n.k ambao wanahusishwa katika mada inayorejelewa
katika hotuba hiyo.
Muundo wa Hotuba
Hutuba
inakuwa na muundo ufuatao:
Anwani
Anwani,
mada au kichwa cha hotuba hurejelea mada ya hotuba. Pia mada inaweza kutaja
hadhira.
- Hotuba
ya Waziri wa Afya kuhusu madhara ya ukimwi kwa wananchi.
- Hotuba
ya Mwalimu Mkuu kwa Wazazi
Utangulizi
- Anza
hotuba yako kwa kuwatambua waliohudhuria mkutano (hadhira).
- Wataje
kwa majina/vyeo vyao kuanzia yule wa cheo cha juu hadi wa chini, mabibi na
mabwana. Kumbuka kwamba hauhitajiki kuwasalimia. Kuwatambua kwa majina
pekee kunatosha.
- Jitambulishe
kwa hadhira yako hasa ikiwa unazungumzia hadhira isiyokujua au wageni.
- Tanguliza
mada yako.
Kwa mfano:
Waziri wa Kilimo, Mkuu wa Wilaya, Mhe. Mbunge, wanachama wa kikundi hiki cha Mazingira, mabibi na mabwana. Ni matumaini yangu kwamba nyote mu buheri wa afya. Mimi ni mwakilishi wa Kikundi cha Mazingira na jioni ya leo kuna jambo muhimu ambalo ningependa sote tulifahamu ili kuboresha mazingira yetu kwa …
Kiini
- Hakikisha
kuna mtiririko wa hoja kuanzia mwanzo hadi mwisho
- Ujumbe
wako wote unapaswa kuwa katika usemi halisia wala si wa taarifa.
Tamati
- Hakikisha
kwamba mwisho wa hotuba yako unatambulika.
- Unaweza
kumaliza kwa shukurani
UANDISHI WA RISALA
Risala
ni hotuba fupi inayosomwa mbele ya kiongozi kwa niaba ya kundi fulani la watu
hasa hasa wanafunzi, wafanyakazi, washiriki, wanachama, mafundi n.k ili kutoa
maelezo ya haja zao mbalimbali na mahitaji yao au kuonyesha msimamo wa kundi
hilo kwa kiongozi.
Muundo wa Risala
Utanguizi
- Cheo
cha kiongozi anayehusika
- Kundi
linalowakilishwa
Kiini
- Maelezo
ya hali halisi ya maswala na msimamo wa kundi linalowakilishwa.
- Mapendekezso
na hatua zinazotakiwa kuchukuliwa.
Hitimisho
- Shukrani
Tanbihi: Kama vilivyosemwa awali risala ni
hotuba fupi lakini inachukua mambo muhimu tu na kuyaeleza. Hivyo risala yenyewe
huwa ni maelezo ya muhtasari kwa jambo linalohitaji maelezo marefu Katika
hotuba. Utungaji wa risala unahitaji uangalifu sana na lugha ya heshima iliyo
wazi kueleweka kwa kiongozi.
Mfano wa Risala:
Ndugu
Mgeni rasmi, Walimu, Wanafunzi wenzetu, Wazazi, Wageni waalikwa, Mabibi na
Mabwana.
Kwa
niaba ya wanafunzi wa kidato cha nne, tunayo heshima na furaha kubwa ,
kukukaribisha ili ushiriki nasi katika siku hii muhimu na kusikia mafanikio
mbalimbali kwa kipindi chote cha masomo yetu hapa shuleni.
Shukrani
zetu za pekee na za dhati ziende kwa uongozi mzima wa Shule na walimu wetu wote
kwa jinsi walivyojitoa kwa moyo wa kutufundisha, hivyo tumefundishika vyema;
kwasababu tupo tofauti sana na tulivyokuja hapa mwezi januari 2009.
Ndugu
mgeni rasmi, tulianza kidato cha kwanza tukiwa wanafunzi 120; wasichana 60 na
wavulana 60. Mpaka leo tunapohitimu tupo wanafunzi 90; kati yao wavulana ni 43,
na wasichana 47. Wengine wameshindwa kuhitimu nasi siku ya leo kutokana na
sababu mbalimbali zikiwemo utoro, ujauzito na kuhama shule. Tunamshukuru
Mwenyezi Mungu mwingi wa Rehema wa Baraka kwa ulinzi wake kwetu hadi leo hii
tunahitimu kidato cha nne.
Ndugu
mgeni rasmi, elimu hii ya kidato cha nne imetupatia msingi mzuri wa kujiunga na
Elimu ya juu, pia imetujengea uwezo mzuri wa kujitambua na kufikiri, kufanya
kazi vizuri na kufanya maamuzi sahihi; pia imetuwezesha sisi wanafunzi kupata
elimu ya mambo mbalimbali kupitia masomo tunayo fundishwa hapa shuleni, mfano;
tumepata elimu ya uraia, historia ya mambo mbalimbali katika nchi yetu na dunia
kwa ujumla, pia tumeweza kupata uelewa kuhusu afya na magonjwa, usalama katika
mazingira yetu, Kilimo, Maumbile ya nchi, hali ya hewa, misitu, na viwanda.
Vilevile tumeelewa umuhimu wa kusoma vitabu mbalimbali kwa lengo la kupata
ujuzi wa kuinua uchumi wetu wa taifa.
Ndugu
mgeni rasmi, mafanikio hayo yamepatikana kwasababu ya ushirikiano mzuri kati
yetu na walimu wetu. Tangu tujiunge na shule hii tukiwa kidato cha kwanza
tumefanya majaribio na mitihani ya mara kwa mara jambo lililo tusaidia kuinua
taaluma yetu.Tunawashukuru sana walimu wetu, tuna waahidi kufanya vizuri katika
mitihani yetu ya Taifa ya kidato cha nne mwaka huu, na Mungu awabariki sana.
Ndugu
mgeni rasmi, tumepata changamoto mbalimbali wakati wa maisha yetu ya kielimu
hapa shuleni, kama ifuatavyo;
Ndugu
mgeni rasmi, tuna changamoto ya upungufu wa vitabu vya kiada na ziada; hii imepelekea
kushindwa kujisomea vizuri, kwani kitabu kimoja kinatumiwa na wanafunzi zaidi
ya ishirini (20).
Ndugu
mgeni rasmi, changamoto nyingine ni upungufu wa vifaa vya maabara, hii
inapelekea kuchangia kifaa kimoja, hivyo tuna tumia muda mwingi sana kujifunza
na kumuelewa mwalimu.
Ndugu
mgeni rasmi, pia kuna changamoto ya upungufu wa walimu, hasa wa masomo ya
sayansi; hii imepelekea kutomaliza ‘syllabus’ kwa wakati.
Ndugu
mgeni rasmi, pia kuna changamoto ya upungufu wa samani za shule, kama vile;
madawati kwa ajili ya wanafunzi, viti na meza kwa ajili ya walimu; hii
imepelekea baadhi ya wanafunzi wenzetu kukaa wawili kwenye dawati moja.
Ndugu
mgeni rasmi, maji ni changamoto hapa shuleni, kwani shule haina kisima cha
maji, hii imepelekea shule kununua maji kwa gharama kubwa, ambayo hayatoshelezi
mahitaji ya shule, kama vile usafi; hususani kwa upande wa vyoo, bila kuwa na
maji ya kutosha tutapata magonjwa ya mlipuko, kama vile kipindupindu.
Ndugu
mgeni rasmi, changamoto ya vifaa vya michezo; kama unavyojua kuwa michezo ni
afya, shule yetu ina upungufu mkubwa wa vifaa vya michezo kama vile; mipira ya
miguu, pete na mikono, pia hatuna milingoti ya chuma kwaajili ya magoli ya
viwanja vya michezo yote tunayocheza hapa shuleni.
Ndugu
mgeni rasmi, tunashukuru uongozi wa shule hii, walimu na wazazi ambao wamekuwa
mstari wa mbele katika kuchangia maendeleo ya shule yetu; kwa upande wa masomo
ya sayansi; shule imeweza kutenga chumba kimoja cha darasa kitumike kama
maabara japo kuwa kuna upungufu mkubwa wa vifaa.
Ndugu
mgeni rasmi, tunayo matumaini kwamba maombi yetu umeyasikiliza na
utayaatekeleza, maana tunajua kwamba wewe unaweza kupitia Hlimashauri unayo
isimamia, asante sana.
Mwisho
tunaomba msamaha wa dhati toka moyoni mwetu kwa Walimu, Wanafunzi wenzetu na Wazazi
pale tulipoenda kinyume na matazamio yenu, kwani watu wakiishi pamoja tofauti
lazima ziwepo, tunatumaini mtapokea msamaha wetu, nasi hatuna jambo lolote baya
kwenu.
Ndugu
mgeni rasmi, tuna kushukuru sana kwa kufika katika Mahafali yetu, kwani tunatambua
kuwa unamajukumu mengi ambayo umeyaacha na kuwepo hapa kwaajili yetu.
Kuandika Risala |
UANDISHI WA KUMBUKUMBU
ZA MIKUTANO
Kumbukumbu
za mikutano ni rekodi zinazowekwa na katibu wa mkutano wakati mkutano
unapoendelea ili kuhifadhi yanayojadiliwa na kukubaliana katika mkutano huo.
Katibu anapaswa kufuatilia mtindo maalum wa kuandika kumbukumbu hizo kulingana
na mpangilio katika mkutano.
Mambo ya Kuzingatia
katika Uchukuaji wa Kumbukumbu za Mikutano
Mambo
ya kuzingatia katika uandishi wa kumbukumbu ni kama yafuatayo:
1. Kichwa cha
kumbukumbu –
Kichwa cha kumbukumbu kinapaswa kutaja mambo yafuatayo: Ni mkutano wa akina
nani? Unaandaliwa wapi? Unaandaliwa lini? Unaanza saa ngapi? Mfano wa Kichwa
cha Kumbukumbu: Kumbukumbu za Mkutano wa Shirika la Msalaba Mwekundu Shuleni
ulioandaliwa tarehe saba Agosti 2001 katika Ukumbi wa Mikutano kuanzia saa Tisa
alasiri.
2. Waliohudhuria – Andika orodha ya wote waliofika
kwenye mkutano huku kuanzia na yule mwenye cheo cha juu zaidi hadi kwa
wanachama. Pia onyesha vyeo vyao.
3. Waliotoa Udhuru -Hawa ni wale walioomba ruhusa
kutohudhuria mkutano
4. Waliokosa
kuhudhuria -
Hawa ni waliokosa kuhudhuria mkutano, bila kutoa udhuru)
5. Waalikwa - Hawa ni wageni walioalikwa katika
mkutano, k.v mlezi wa chama, afisa wa kiutawala, n.k)
Kumbukumbu
KUMB
1
|
Kumbukumbu
ya kwanza huwa ni kufunguliwa kwa mkutano na ujumbe kutoka kwa mwenyekiti.
|
KUMB
2
|
Kusomwa
kwa kumbukumbu za mkutano uliotangulia na kuthibitishwa kwa kumbu kumbu hizo
kwa kutiwa saini.
|
KUMB
3
|
Maswala
yanayoibuka kutokana na kumbu kumbu zilizosomwa. (Kumbuka kutaja nambari ya
kumbu kumbu hizo)
|
KUMB
kuendelea
|
Maswala
katika ajenda
|
KUMB
ya Mwisho
|
Maswala
mengineyo yasiyokuwa kwenye orodha ya ajenda.
|
Tamati
|
Kufungwa
kwa mkutano. Taja mkutano ulifungwa saa ngapi; mkutano ujao utakuwa tarehe
ngapi; kisha acha nafasi ya kuthibitishwa kwa kumbu kumbu hizo katika mkutano
utakaofuatia.
|
Mfano:
KUMBUKUMBU
ZA MKUTANO WA CHAMA CHA KISWAHILI ULIOANDALIWA KATIKA CHUMBA CHA MIJADALA
TAREHE 24 JUNE 2013 KUANZIA SAA TATU ASUBUHI
Waliohudhuria
- Teddy
Mbogela – Mwenyekiti
- Vaileth
Matiko – Mweka hazina
- Iliashibu
Masatu – Mkuu wa utafiti
- Funk
Kiduku – mwanachama
- Meta
Mkorofi – katibu
Waliotuma
Udhuru
- Bahatika
Mashauri – Naibu Mwenyekiti
- Ponea
Kamgazi – Msimamizi wa Mijadala
Waliokosa
Kuhudhuria
- Zebedayo
Chisege – Spika
- John
Kumbikumbi – mwanachama
Waalikwa
- Mnoko
Nokwe – Mwanahabari
- Dkt.
Fikirini– Mlezi wa Chama.
Ajenda
- Uchapishaji
wa jarida la Kiswahili
- Shindano
la kuandika insha.
- Kusajili
wanachama wapya
KUMBUKUMBU 3/04/14 – KUFUNGULIWA KWA MKUTANO
Mwenyekiti
aliwakaribisha wanachama wote na baada ya kuwatambulisha wageni, akawaomba
washiriki wawe huru kuchangia katika ajenda mkutano huu ili kuboresha chama.
KUMBUKUMBU
7/04/14 – KUREJELEA KUMBUKUMBU ZA MKUTANO ULIOPITA
Katibu
alisoma kumbukumbu za mkutano wa mwezi Machi. Kumbukumbu zilikubaliwa na
wanachama wote na kuthibitishwa na mwenyekiti pamoja na katibu kwa kutia saini.
KUMBUKUMBU
10/04/14 – MASWALA IBUKA KUTOKANA NA KUMBUKUMBU ZILIZOSOMWA
Mweka
hazina alifahamisha mkutano kwamba aliongea na mkuu wa idara ya Kiswahili
kuhusu ufadhili kama tulivyokuwa tumekubaliana katika KUMB 9/03/10 ya mkutano
uliopita.
KUMBUKUMBU
12/04/14 – HAFLA YA KISWAHILI
Iliripotiwa
kwamba hafla ya Kiswahili ambayo wanachama walikuwa wamealikwa kuhudhuria
katika Shule ya Sakata Academy haingeweza kufanyika kutokana na tamasha la
muziki lilizokuwa linaendelea katika shule hiyo. Wanachama waliokuwa
wamejitayarisha kwa mashairi waliombwa kuendelea kujifunza ili wayawasilishe
muhula wa pili.
KUMBUKUMBU
15/04/14 – UCHAPISHAJI WA JARIDA LA KISWAHILI
Wanachama
walikubaliana:
- Kwamba
chama kitaanza kuchapisha jarida la Kiswahili
- Kwamba
jarida litakuwa likichapishwa mara moja kila muhula na kuuzwa shuleni
- Kwamba
kila mwanachama atachangia katika kuandika makala na kuuza nakala za
jarida hilo.
- Kwamba
paneli ya wahariri lingeundwa ili kuongoza idara ya uchapishaji
- Kwamba
hazina ya chama ina fedha za kutosha kuzindua uchapishaji huo.
KUMBUKUMBU
17/04/14 – SHINDANO LA KUANDIKA INSHA
Kila
muhula wa pili, chama huandaa shindano la kuandika insha ambalo wanafunzi wote
hushiriki. Insha zilizopendekezwa mwaka huu ni:
- “Jadili
chanzo cha migomo shuleni na namna ya kusuluhisha.”
- …
… … … … … … … …
- …
… … … … … … … …
- …
… … … … … … … …
KUFUNGWA
KWA MKUTANO
Mkutano
ulifungwa saa kumi na nusu, baada ya maswala yote kujadiliwa. Mkutano
unaofuatia ulipoangwa kuwa tarehe ishirini mwezi Mei, katika Ukumbi wa Muziki.
KUTHIBITISHWA
KWA KUMBUKUMBU
______________
|
_____________
|
Mwenyekiti
|
Katibu
|
Tarehe:________
|
Tarehe:________
|
EmoticonEmoticon