Join Our Groups
TOPIC 6: UANDISHI WA
INSHA
Uandishi Wa Insha
Uandishi
ni kitendo cha kupangilia maneno katika maandishi. Mada hii inazungumzia
uandishi wa insha za wasifu kwa umahususi wake. Kabla ya kuanza uandishi
utajifunza mambo muhimu yanayopaswa kuzingatiwa katika uandishi wa insha kwa
ujumla. Utaelewa muundo wa insha na mwisho utajifunza juu ya dhana ya insha ya
wasifu na namna inavyoandikwa na mwisho kabisa utaangalia mfano wa insha ya
wasifu.
Insha za Wasifu
Insha
ya wasifu ni ile ya kutoa maelezo juu ya jinsi mtu au kitu kilivyo, tabia,
vitendo na mandhari (sura ya mahali jinsi panavyoonekana). Mambo muhimu katika
insha ya wasifu ni: sura, rangi, umbo, vipimo, tabia, na kadhalika. Insha hizi
zinaweza kuongelea kitu chochote kile, inaweza kuwa ni mnyama, mtu, Shule, nchi
na kadhalika.
Hatua za Uandishi wa
Insha
Kabla
ya kuanza kuandika insha, ni muhimu sana uamue unataka kuandika juu ya nini.
Inafaa uchague ile mada iliyo rahisi kwako kuweza kujieleza kikamilifu na kwa
urahisi. Kama unaandika insha za kufanyia mazoezi ni heri uchague mada zenye
habari ambazo unazielewa.
Iwapo
hulijui au hulielewi jambo, ufanye uchunguzi kwanza. Ukisha kupata habari
muhimu ndipo baadaye uandike insha yako kulingana na jinsi unavyoijua na jinsi
unavyoikumbuka habari inayohusika.
Katika
mtihani ni muhimu uyasome maagizo kwa makini. Kwa mfano, maagizo yanaweza kuwa:
Chagua mojawapo ya habari zifuatazo kisha uandike insha isiyopungua kurasa
mbili za karatasi za majibu.
Au:
Chagua
mojawapo ya habari hizi kisha uandike insha ya maneno yasiyopungua 400.
Ni
heri uandike insha nzuri ya kiwango kinachotakiwa kuliko ndefu (zaidi ya maneno
400) ambayo haitakuwa na mambo muhimu hadi mwisho, na pengine yenye makosa na
uchafu mwingi kupindukia. Ni muhimu ikumbukwe jinsi insha ilivyo ndefu, hasa
katika mtihani, ndivyo idadi ya makosa inavyozidi kuongezeka.
MUUNDO WA INSHA
Katika
uandishi wa insha, muundo wake unakuwa na vitu vifuatavyo:
1. Kichwa cha insha; kichwa cha insha hudokeza kile
ulichokijadili katika insha yako. Kwa mfano: Madhara ya matumizi ya madawa ya
kulevya n.k
2. Utangulizi; Mambo yaliyopo katika utangulizi
ni pamoja na kutoa fasili ya maneno muhimu na kuelezea kwa muhtasari mambo
ambayo utakwenda kuyajadili katika insha yako.
3. Kiini cha insha; katika kiini ndipo kuna maelezo ya
kina juu ya kile unachokijadili katika insha yako, maelezo haya yanakuwa katika
aya kadhaa kulingana na idadi ya hoja ulizonazo katika mjadala wako.
4. Hitimisho; hapa ndipo kuna muhtasari wa kile
kilichojadiliwa katika kiini cha insha au inaweza kuwa ni msimamo juu ya kile
kilichohadiliwa katika insha.
Hebu soma mfano ufuatao wa insha ya
wasifu:
Mfano 1
SHULE YANGU
Shule
yangu inaitwa Shule ya Sekondari ya Mwananchi. Ni shule ya zamani iliyoanzishwa
siku ya Ijumaa, tarehe 5 Agosti 1966 na Mheshimiwa Donna Matembele, aliyekuwa
diwani wa kata ya Masuba.
Shule
hii ambayo ni maarufu sana ipo katika Tarafa ya Mkunazini. Imejengwa katika
uwanja wa hekta kumi na mbili. Ina madarasa kumi na mawili ya vidato vinne vya
mikondo mitatu kila kimoja. Ina wanafunzi mia tano na wanne badala ya idadi
halali ya wanafunzi mia nne themanini. Ni shule inayopendwa sana.
Wanafunzi
wa kike ni mia mbili na watatu na wa kiume ni mia tatu na mmoja. Walimu ni
thelathini na mmoja. Jamii hii inapendana sana. Wanafunzi wana imani kubwa sana
na walimu wao. Walimu huwahimiza wawe wanafanya bidii katika kazi na masomo kwa
ujumla.
Wanafunzi
hukadiria ugumu wa mazoezi wapewayo. Yale wayaonayo kuwa ni rahisi wao
hujifanyia. Yale magumu kidogo hushughulikia kwa pamoja kwa kusaidiana wenyewe
kwa wenyewe. Walimu hushirikishwa tu wakati wa mazoezi tata.
Shule
ya Sekondari ya Mwananchi ni ya kuvutia sana. Ina miti mingi sana ya matunda.
Ina maua ya aina aina. Kutokana na nidhamu na uwajibikaji matunda hukomaa ndipo
yatumiwe kwa mpango wakati wa chakula.
Heshima
imethaminiwa mno na wanafunzi. Wanaheshimiana na kuwaheshimu walimu wao. Kwao
heshima ni utiifu na uzingativu. Kutii na kuzingatia mambo waambiwayo na walimu
ndicho kipimo cha heshima.
Katika
shule yangu wanafunzi tuko kama paka. Paka hamtumi mtu nyama lakini atunukiwapo
kipande hawezi kumruhusu yeyote kukigusa. Nasi tutunukiwapo nafasi yoyote ya
kusoma hatumruhusu mtu yeyote kutupokonya nafasi hiyo.
Wanafunzi
wa shule wana sare zao za kuvutia wazivaazo kiungwana kabisa. Sare hizo ni
sweta ya bluu, shati au blauzi ya samawati, tai ya rangi ya damu ya mzee,
suruali ndefu au sketi ya kijani kibichi, viatu vyeusi vya soli ndogo na
visigino vifupi.
Katika
shule yetu kuna uhusianao mwema baina ya walimu, wazazi, Chama cha Wazazi na
Walimu (CHAWAWA) na Baraza la Shule. Kamati ya CHAWAWA na Baraza la Shule
huanzisha miradi na kuitekeleza haraka kutokana na wazazi kuiunga mkono.
Kwa
muda mrefu sasa matokeo ya mitihani yamekuwa ya kuridhisha kabisa. Na si hayo
peke yake. Wanafunzi washirikipo katika michezo ya mpira, ya riadha na
matamasha ya muziki takribani mara zote huibuka washindi.
Kwa
ufupi shule yangu ni ya mafanikio mengi.
Mshindi wa Kuandika Insha akipewa zawadi |
Mambo muhimu ya kuzingatiwa katika insha hii ya wasifu:
1.
KICHWA (Shule yangu)
2.
MAELEZO KAMILI yenye
3.
JINA la shule
4.
HISTORIA ya shule
5.
MAZINGIRA ya shule
6.
IDADI ya wanafunzi na walimu
7.
HALI ya wanafunzi
8.
MAFANIKIO ya shule.
9.
HITIMISHO lenye sifa ya jumla.
Zoezi 1
Tofautisha
insha za kisanaa na zisizo za kisanaa
EmoticonEmoticon