Join Our Groups
TOPIC
4: UHAKIKI WA KAZI ZA FASIHI ANDISHI
Fasihi
andishi ni tawi la fasihi linalotumia sanaa ya maneno kufikisha ujumbe kwa
hadhira kwa njia ya maandishi. Zipo aina nyingi za fasihi andishi, miongoni mwa
hizo ni pamoja na hadithi fupi, riwaya, tamthiliya na mashairi.
Maana ya Uhakiki
Uhakiki ni kitendo cha kutathimini, kueleza, kuainisha na kutoa maoni juu
ya kazi fulani ya fasihi kwa kuongozwa na kaida maalum. Hii ina maana kwamba
uhakiki wa kazi za fasihi hautoki katika ombwe, kuna kanuni na taratibu mbalimbali
zinazoongoza kufanya uhakiki, na hii ndio sababu kuna nadharia kadha wa kadha
za uhakiki wa kazi za kifaishi. AU kwa lugha rahisi tunaweza kusema, uhakiki ni
uchambuzi wa kina wa kazi za fasihi kama vile riwaya, tamthiliya na mashairi
kwa lengo la kufafanua vipengele vya fani na maudhui.
Misingi ya
Uhakiki
Kwa ujumla mhakiki wa kazi za fasihi anapofanya uhakiki wa kazi za
kifasihi, huwa analenga vipengele viwili. Pengine analenga kuhakiki fani ya
kazi husika au maudhui ya kazi hiyo na wakati mwingine vyote viwili. Kwa
hiyo kupitia vipengele hivi ndipo atachambua vitu vingi kama vile ujumbe,
falsafa, matumizi ya lugha, dhamira, mandhari na kadhalika.
Kuhakiki Fani
Katika utunzi wa kazi za kifasihi, Fani hutumika kama nyezo ya kuwasilisha
mawazo ya mwandishi kwa njia ya kisanaa zaidi. Fani ni mbinu anayoitumia
mwandshi ili kufikisha ujumbe kwa watu aliowakusudia.
Vipengele vya fani ni pamoja na wahusika, mandhari, lugha, muundo na mtindo.
Mtindo
Mtindo ni mbinu ya kipekee kifani na kimaudhui, zinazotofautisha msanii
mmoja na mwingine. Kwa mfano, namna msanii anavyotumia lugha, anavyoteua
msamiati, namna anavyosimulia hadithi yake (anaweza kutumia nafsi ya kwanza, ya
pili au ya tatu). Kwa mfano katika riwaya ya “Barua Ndefu kama hii” iliyoandikwa
na Mariama Ba ametumia mtindo wa barua ya kirafiki kuanzia mwanzo hadi mwisho,
hii pia inaonesha mtindo wake wa kipekee.
Muundo
Muundo ni mpangilio wa kiufundi anaoutumia mwandishi katika kupangilia kazi
yake. mpangilio na mtiririko wa kazi ya fasihi, kwa upande wa visa na matukio.
Kuna aina mbili za kupangilia matukio
1. Msago; hii ni namana ya moja kwa moja ya
kusimulia matukio, yaani kuanzia tukio la kwanza hadi la mwisho kwa namna
yalivyotukia. Huu ni muundo wa moja kwa moja.
2. Urejeshi; huu ni usimuliaji wa kurukaruka
hatua, yaani msimuliaji anaweza kuanzia katikati, akaja mwisho na kumalizia na
mwanzo
Wahusika
Wahusika; ni watu au viumbe ambavyo mwandishi wa fasihi huwatumia ili
kufanikisha ujumbe kwa jamii husika. Katika kazi ya fasihi mwandishi huwagawa
wahusika katika makundi mawili yaani wahusika wakuu na wahusika wadogo.
Wahusika wakuu ni wale ambao wanajitokeza kuanzia mwanzo mpaka mwisho wa
kazi ya fasihi. Wahusika wadogo ni wale wote ambao wanajitokeza sehemu
mbalimbali katika kazi ya fasihi kwa mfano, mwanzoni mwa kitabu hadi mwishoni
mwa kitabu.
Wahusika hawa wawe ni wakuu au wadogo wanaweza kugawanyika katika makundi
yafuatayo:
1. Mhusika mviringo ni mhusika ambaye anabadilika kitabia na kimawazo kulingana na hali
halisi ya maisha. Kwa mfano wanaweza kuanza kama watu wema lakini hali ya
maisha ikawabadilisha na kuwa watu wabaya au wanaweza kuanza kama watu wabaya
na hali ya maisha ikawabadilisha na kuwa watu wema.
2. Mhusika bapa ni mhusika ambaye habadiliki kulingana na hali halisi ya maisha. Mfano;
kama ni mwema basi atakuwa mwema kuanzia mwanzo wa hadithi hadi mwisho na kama
ni mbaya basi atakuwa mbaya kuanzia mwanzo wa hadithi hadi mwisho.
3. Mhusika shinda yuko
katikikati ya mhusika papa na mviringo. Huongozwa na matendo ya hao wahusika
wawili. Hajitokezi na msimamo wake imara.
Mandhari
Mandhari; hii ni sehemu ambayo matukio ya hadithi au masimulizi hutokea.
Mandhari huweza kuwa halisi kama vile baharini, njiani, msituni, kijijini,
mijini au ya kufikirika kama vile kuzimu, mbinguni, peponi n.k.
Lugha
Lugha ndio nyenzo kubwa ya msanii katika kazi za fasihi, miongoni mwa
vipengele vya lugha ni tamathali za semi pamoja na semi.
Fani za Lugha
1. Tanakali za Sauti: Ni mbinu ya kutumia maneno yanayoiga sauti au hali fulani au namna kitendo
kilivyofanyika.
2. Tashbiha: Hii ni mbinu ya lugha
inayolinganisha vitu au hali mbili tofauti kwa kutumia maneno ya kulinganisha;
‘kama’, ‘mithili ya’, ‘sawa na’, ‘ja’. mfano, Mwembamba kama sindano.
3. Tashihisi: Hii ni mbinu ya kupatia
kitu kisicho hai sifa za kiumbe mwenye uhai (sifa za kibinadamu). Mfano,
"Sungura aliposhindwa, akasema sizitaki hizi mbichi".
4. Takriri: Ni mbinu ya kurudiarudia
neno moja au kifungu cha maneno ili kusisitiza ujumbe fulani. Mfano, alikimbia,
alikimbia, alikimbia hadi akashika nafasi ya kwanza.
5. Ukinzani: Ukinzani ni mbinu ya
kusisitiza ujumbe kwa kuambatanisha maneno ya kinyume au yanayokinzana.
6. Sitiari: Ni mbinu ya kulinganisha
vitu viwili moja kwa moja kwa kutumia kiungo ‘ni’ ama ‘kuwa’. Mfano; Maisha ni
mlima, juma ni mwamba.
7. Taswira: Ni matumizi ya lugha/maneno
yanayojenga picha ya hali au jambo fulani kwa msomaji.
8. Taashira: Ni matumizi ya lugha ya
ishara kuwakilisha ujumbe fulani. Jina au kitu fulani kinatumika kumaanisha
kitu kingine chenye uhusiano na kile kilichotumiwa.
9. Jazanda: Ni kulinganisha vitu viwili
moja kwa moja bila kutumia viunganishi.
10. Majazi: Majazi ni pale tabia za
wahusika zinapoambatana na majina yao halisi.
11. Lakabu: Ni mbinu ya mhusika
kupewa/kubandikwa jina na wahusika wengine ama yeye mwenyewe kujibandika jina
linalooana na tabia/sifa zake.
12. Chuku: Ni kutumia maneno
yaliyotiliwa chumvi ili kusisitiza ujumbe fulani au kusifia kitu, kutilia
Chumvi.
Semi
Ni fungu la maneno linapotumika kutoa maana nyingine, badala ya ile ya
maneno yaliyotumika. Semi hutumika kuficha ukali wa maneno au kupamba lugha.
Kuna aina mbili za semi:
- Nahau – ni usemi unaotumia maneno ya
kawaida kwa lengo la kufikisha maana iliyotofauti na maana ya kawaida ya maneno
hayo. Nahau huwa na vitenzi.
- Misemo – ni semi fupifupi ambazo hutumiwa
mara kwa mara kwa lengo la kuleta maana maalumu. Misemo haina vitenzi.
1. Maswali ya Balagha: Tashititi au maswali ya balagha ni maswali yanayoulizwa na msimulizi
au mhusika ambayo hayahitaji jibu.
2. Uzungumzi Nafsiya: Mhusika hujizungumzia, ama kwa kuongea au kuwaza, bila kukusudia
kusikika na yeyote.
3. Ritifaa: Mbinu ya kuzungumza na mtu
aliyekufa (au asiyekuwepo) kana kwamba yuko pamoja nawe.
4. Kuchanganya Ndimi: Kuweka maneno yasiyo ya Kiswahili
katika sentensi ya Kiswahili. Mfano, "alisimama kwanza kwa muda, before he
went aliniambia nisimwambie mtu yeyote yule, you know!"
5. Kuhamisha Ndimi: Ni
kuingiza sentensi ya lugha nyingine katika kifungu cha lugha ya Kiswahili.
Kinyume na Kuchanganya ndimi (ambapo mwandishi huchanganya maneno katika
sentensi moja, katika kuhamisha ndimi, sentensi kamilifu ya lugha nyingine
hutumika miongoni mwa sentensi za Kiswahili sanifu. Mfano: Kazi hii ni ngumu
sana, sitaweza kuifanya. People are trying to convince me to stay here but I
think I can't, I must go!
6. Methali: Methali ni misemo ya hekima
yenye maana iliyofumbwa. Mhusika, mwandishi wa fasihi anaweza kutumia methali
kupitisha ujumbe.
Mbinu nyingine za Kisanaa
1. Kinaya: Kinaya ni mambo katika
sanaa kuwa kinyume na matarajio ya hadhira.
2. Kejeli; Kejeli ni mbinu ya sanaa
inayotumia maneno kudharau au kukemea kitendo au mtu fulani.
3. Taharuki; Taharuki ni mbinu ya
kusimulia au kuandika riwaya/hadithi kwa kufanya hadhira na/au wahusika wajawe
na hamu ya kutaka kujua kitakachotokea baadaye; hamu ya kutaka kuendelea
kusoma/kusikiliza. Baadhi ya hadithi huishia kwa taharuki na kuilazimisha
hadhira yake ijikamilishie au ibaki ikijiuliza maswali.
4. Sadfa; Sadfa ni kugongana kwa vitendo
viwili vinavyohusiana kana kwamba vilikuwa vimepangwa, japo havikuwa
vimepangiwa.
5. Kisengere Nyuma; Mwandishi
‘hurudi nyuma’ na kuanza kusimulia kisa kilichokuwa kimetendeka kabla ya
alichokuwa akisimulia. Aidha, mwandishi hubadilisha wakati wa masimulizi na kuwa
wakati wa kisa hicho. Hutumika sana kuonyesha mhusika anapokumbuka kitu, au
kutupatia msingi wa jinsi mambo yalivyoanza.
6. Kisengere Mbele; Mwandishi
anapobadilisha wakati na kusimulia mambo yatakavyokuwa siku za usoni; au
kutumia lugha isiyo moja kwa moja kutabiri yatakayojiri. Utabiri.
KUHAKIKI MAUDHUI
Maudhui katika kazi ya fasihi ni jumla ya mawazo yote yanayozungumzwa
pamoja na mtazamo wa mwandishi juu ya mawazo hayo. Maudhui hujumuisha mawazo
pamoja na mafunzo mbalimbali yaliyomsukuma msanii hadi akatunga na kusanii kazi
fulani ya kifasihi. Vipengele vya maudhui ni pamoja na dhamira, migogoro,
falsafa ujumbe na msimamo.
1. Dhamira; hili ni wazo kuu au mawazo
mbalimbali yanayojitokeza katika kazi ya fasihi. Dhamira ni sehemu tu ya
maudhui na aghalabu dhamira kuu ndio hujenga kiini cha kazi ya fasihi. Dhamira
zimegawanyika katika makundi mawili, kuna dhamira kuu na dhamira ndogondogo.
2. Migogoro; hii ni mivutano na
misuguano mbalimbali katika kazi za fasihi. Migogoro inaweza kuwa kati ya wahusika,
familia zao, matabaka yao, au hata katika nyadhifa mbalimbali. Vilevile
migogoro yaweza kuwa ya kiuchumi, kijamii, mogogoro ya nafsi, na migogoro ya
kisiasa ambayo hujitokeza katika mitazamo tofauti kulingana na mtiririko wa
visa na matukio yanavyopangwa na mwandishi.
3. Ujumbe; mwandishi anapoandika kazi
yake huwa na ujumbe ambao hutaka uifikie jamii aliyoikusudia. Ujumbe katika
kazi fasihi ni mafunzo mbalimbali ambayo hupatikana baada ya kusoma kazi ya
fasihi. Katika kazi ya fasihi dhamira kuu hubeba ujumbe wa msingi na dhamira
ndogondogo hubeba ujumbe ambao husaidia kuujenga au kuupa uzito zaidi ujumbe wa
msingi.
4. Msimamo; katika kazi ya fasihi,
mawazo, mafunzo na falsafa ya msanii hubainisha msimamo wake kuhusu masuala
mbalimbali ya kijamii. Msimamo ni ile hali ya mwandishi kuamua kufuata na
kushikilia jambo fulani. Jambo hili huweza kukataliwa na wengi lakini
akalishikilia tu. Msimamo ndio huweza kuwatofautisha wasanii wawili au zaidi
wanaoandika kuhusu mazingira yanayofanana. Kwa mfano, katika tamthilia ya “Pesa
zako zinanuka” mwandishi anamsimamo wa kimapinduzi kwani amejadili matatizo
yanayochangia kukwama kwa ujenzi wa jamii mpya.
5. Falsafa ni mawazo ya busara yenye
kutawaliwa na misingi mahususi juu ya asili na maana ya ulimwengu na maisha ya
mwanadamu. Ni msimamo wa msanii katika maisha juu ya utatuzi wa matatizo katika
jamii. Falsafa ya mwandishi inaweza kujulikana kwa kusoma kazi zake zaidi ya
moja.
6. Mtazamo ni hisia au uelewa wa
mwandishi juu ya jambo fulani. Kwa mfano anaweza kutazama jambo fulani kwa
mtazamo wa kidini, au anaweza kutazama jambo fulani kwa mtazamo wa kisiasa au
kisayansi.
7. Mafunzo; ni mawazo ya kuelimisha
yanayopatikana katika dhamira mbalimbali za kazi ya fasihi.
Kufaulu na Kutofaulu kwa Mwandishi
Kufaulu au kutofaulu kwa mwandishi kunategemea jinsi alivyoweka uwiano
mzuri kati ya fani na maudhui kwa namna ambavyo inaleta uhalisia. Mfano, endapo
msanii atakuwa na mhusika Mkongo lakini akawa anazungumza kiswahili kilichojaa
misemo na nahau alafu kimenyooka kama mtu wa pwani itakuwa vigumu kusema
amefaulu kwani hakuna uwiano mzuri kati ya mhusika mwenyewe na lugha
anayoitumia. Kiswahili cha Kongo ni tofauti kabisa na kiswahili
kinachozungumzwa na watu wa pwani (Tanzania).
notes are not so complicated
ReplyDelete