Join Our Groups
TOPIC 6: UANDISHI WA INSHA NA MATANGAZO
UANDISHI WA INSHA ZA KISANAA
Insha za kisanaa ni insha zinazoelezea mambo ya kawaida katika jamii lakini
kwa kutumia lugha ya kisanaa. Lugha ya kisanaa ni pamoja na matumizi ya
tamathali za semi, misemo nahau, methali na taswira. Au, Insha ya kisanaa ni
ile inayotumia lugha ya kisanaa yaani yenye tamathali za semi kama vile
sitiari, tashbiha, taniaba na mubalagha. Aidha insha ya kisanaa hutumia mbinu
nyingine za kisanaa kama tashititi, takriri, na tanakali sauti. Vilevile insha
za kisanaa huwa na lugha zenye mvuto na misemo kama nahau, methali na tamathali
za semi.
Muundo wa Insha
Kwa kawaida insha inakuwa na sehemu kuu nne: kichwa cha insha, utangulizi,
kiini na hitimisho.
a) Kichwa cha
insha; Kichwa cha insha hudokeza kile
utachokijadili katika insha yako, hubainisha wazo kuu la mada inayohusika. Kwa
kawaida kichwa cha insha huandikwa kwa sentensi fupi. Mfano; maisha ya
kijijini, mimba za utotoni.
b) Utangulizi;
Mambo yaliyopo katika utangulizi ni pamoja na kutoa fasili ya maneno muhimu
na kuelezea kwa muhtasari mambo ambayo utakwenda kuyajadili katika insha yako.
Utangulizi unakuwa katika aya moja fupi.
c) Kiini cha insha; Katika kiini ndipo kuna maelezo ya kina juu ya kile unachokijadili
katika insha yako, maelezo haya yanakuwa katika aya kadhaa kulingana na idadi
ya hoja ulizonazo katika mjadala wako.
d) Hitimisho; Hapa ndipo kuna muhtasari wa kile kilichojadiliwa katika kiini cha
insha au inaweza kuwa ni msimamo juu ya kile kilichojadiliwa katika insha.
UANDISHI WA MATANGAZO
Tangazo ni taarifa za wazi zinazotoa ujumbe fulani kwa walengwa wanaohusika
na ujumbe huo. Ujumbe unaweza kuwa na lengo la kushawishi, kuarifu, kuelekeza,
na kadhalika.
Vipengele vya Kuzingatiwa katika Uandishi wa
Mtangazo
Malengo ya Matangazo
1. Kutoa taarifa; Lengo mojawapo la matangazo ni kutoa taarifa, mfano wa matangazo yanayotoa
taarifa ni mialiko, tangazo la kifo, alama za barabarani, matangazo ya kazi.
2. Kuonya; Matangazo pia yana lengo la
kuonya, kwa mfano matangazo kama vile ya kutovuta sigara, UKIMWI na kadhalika.
3. Kushawishi; Matangazo pia yana lengo la
kushawishi, matangazo yenye lengo hili mara nyingi ni matangazo ya biashara
ambayo kwa kweli lengo lake ni kushawishi wateja ili wanunue bidhaa zao,
mtangazo ya mialiko hasahasa ya tukio fulani, labda msanii anazindua albamu
fulani na kadhalika.
Jinsi ya Kuandika Matangazo
Ili tangazo liweze kufanikisha kufikia lengo lililokusudiwa kuna mambo
kadhaa ya kufanya; mambo hayo ni kama yafuatayo:
1. Kichwa cha habari; Mara nyingi matangazo yanakuwa na kichwa cha habari, hii inasaidia
kujua kwa haraka kuwa tangazo linahusika na kitu gani.
2. Kuonesha aina ya bidhaa/huduma; Hiki ndicho kiini cha tangazo, hapa tangazo linaonesha ujumbe
uliokusudiwa kufikishwa kwa wahusika, sasa ujumbe huu waweza kuwa ni bidhaa
inayotangazwa au huduma inayotolewa au kazi inayotangazwa au mwaliko unahusu
nini.
3. Anwani; Hapa tangazo linaonesha
mahali ambapo watoa tangazo walipo, yaani ofisi zao zilipo ambapo wahusika wa
tangazo wanaweza kwenda na kuwakuta. Kama ni tangazo la mwaliko basi ni lazima
lionesha shughuli yenyewe itafanyika wapi.
4. Njia za mawasiliano; Kama ni tangazo la biashara au la kazi au la mwaliko ni muhimu kutoa
mawasiliano. Mawasiliano hayo yanaweza kuwa ni namba ya simu, fax, wavuti (kwa
taarifa zaidi), barua pepe.
Mbinu za Uandishi wa Matangazo
Ili tangazo liweze kuvuta umakini wa watu ni lazima liwe na mwonekanao
fulani. Zifuatazo ni mbinu za uandishi wa matangazo.
1. Matumizi ya picha; Matangazo mengi ya biashara huwa yanaambatana na picha, picha hizi hujaribu
kumshawishi mteja aamini kuwa ile bidhaa ni bora na hivyo ni muhimu kuwa nayo
au kuinunua.
2. Maneno machache; Matangazo
hutumia maneno machache kwa lengo la kutomchosha mlengwa lakini wakati huohuo
maneno hayo yana nguvu ya kumshawishi mlengwa.
3. Lugha ya kisanii; Maneno ya kisanii katika matangazo huwa ni mepesi kukumbukwa na huwa
yanaeleweka kirahisi. Kwa mfano, matumizi ya vivumishi, litakuwa ni bonge la shoo, njoo ujinunulie pamba za ukweli, n.k. Matumizi ya mubalagha,
kwa mfano; mtandao unaoongoza Tanzania, mganga bingwa afrika mashariki na kati
n.k
4. Matumizi ya watu maarufu; Matangazo mengi hususani ya biashara hupenda kutumia watu maarufu ili
kuwashawishi walengwa. Kwa mfano kama ni tangazo juu ya bidhaa fulani, huweza
kumwonesha pengine msanii maarufu, miss Tanzania, au mchezajia mpira maarufu.
Sasa mlengwa anapoona kwamba hata mtu maarufu anatumia hiyo bidhaa,
anashawishika na yeye kuitumia
Ubarikiwe kazi iko vzri🙏
ReplyDeleteGood notes.big up
ReplyDeleteNzuri
ReplyDeleteNZURI
ReplyDeleteShukrani
ReplyDelete