Join Our Groups
TOPIC 2: MATUMIZI YA LUGHA KATIKA MIKTADHA MBALI MBALI
REJESTA
Kwa
ujumla tunaweza kufasili rejesta kama mtindo wa lugha kutegemeana na kazi
fulani, muktadha wa matumizi, lengo na uhusiano wa wanaowasiliana. Katika
muktadha rasmi rejesta hurejelea upande mmoja kama vile, msamiati wa kiufundi,
adabu maalum na matumizi ya lugha fasaha, mfano katika elimu, mahakamani na
kadhalika.
Kuwasiliana kwa
kutumia Rejesta
Rejesta za Mitaani
Haya
ni mazungumzo yanayozungumzwa magengeni nayo hueleweka na wazungumzaji wenyewe.
Ni lugha ambayo huchipuka kutokana na kikundi cha watu ambacho ni kidogo. Mfano
wa maneno yanayotumika sana mitaani ni kama vile “Mshikaji” (rafiki) Demu”
(mwanamke) n.k. Kwa ujumla lugha ya mitaani ni lugha isiyo sanifu, ni lugha
iliyojaa maneno ya mitaani ambayo yanaeleweka kwa wazungumzaji wenyewe.
Mazungumzo ya Kwenye
Shughuli Maalum (Rejesta za Mahali)
Mazungumzo
ya kwenye shughuli maalumu hayafanywi kiholela, bali yanafuata taratibu na
kanuni maalum zinazojitokeza katika mazingira haya. Kutokana na kutumiwa kwake
kwa muda mrefu kwenye mazingira yale yale.
Mazungumzo
ya kwenye shughuli maalumu ni kama vile mazungumzo ya:
1.
Maofisini au mahali popote pa kazi
2.
Mahakamani
3.
Hotelini
4.
Hospitalini
5. Msikitini
6.
Kanisani n.k
Hotelini |
Mazungumzo ya mahotelini yana utaratibu wake ambao katika hali ya kawaida inaweza isieleweke.
A: Nani wali kuku?
B:
Mimi
A: Chai moja wapi?
B:
Hapa
Katika
mazungumzo haya A anapouliza “Nani wali kuku”, ana maana kuwa nani anahitaji
kula wali na nyama ya kuku”. Hapa hana maana ya kumwainisha mtu aitwaaye “wali kuku”.
Kwa
upande wa lugha ya mahakamani ni tofauti na lugha ya hotelini. Lugha ya
mahakamani inasisitiza usahihi ili kuondoa migongano miongoni mwa wanaohusika.
Mfano 1
Wakili
wa Utetezi: Nakuuliza jaribio la kutaka kupindua serikali litakuwa kosa la namna
gani katika sheria za Tanzania?
Kamishna
Msaidizi: (Baada ya kupewa kitabu cha sheria za Tanzania na kukisoma) Ni kosa
la uhaini.
Wakili
wa Utetezi: Ulichukua muda mrefu kufikia jibu hili. Washitakiwa wawili
hawahusiani na makosa haya?
Kamishna
Msaidizi: Sijui.
Kimsingi
hii ni hali ya kawaida kabisa katika mahojiano ya mahakamani. Mara nyingi
mahojiano katika mahakama hayaendi haraka sana. Kila mtu anayehusika – hakimu,
mwendesha mashtaka, wakili, mdaiwa, shahidi, n.k. hujieleza kwa wazi wazi bila
kujali urefu wa maelezo.
Rejesta Zinazohusu Watu
Rejesta
zinazohusu watu ni yale mawasiliano yasiyo rasmi, ni yale maongezi ya kawaida
ya kila siku au mazungumzo rasmi; kwa mfano mazungumzo kati ya:
1. Vijana wenye rika moja
2.
Wazee wenyewe
3. Wanawake wenyewe
4.
Wanaume wenyewe
5.
Mwalimu na mwanafunzi
6.
Meneja na wafanyakazi wake
7.
Mtu na mpenzi wake, n.k.
Mazungumzo
miongoni mwa marafiki wa rika moja huzungumza lugha ambayo wao wenyewe
wanaielewa na sio rahisi kwa mtu wa rika lingine kuielewa lugha hiyo.
Mfano 2
'Basi,
Master jana wikiendi ilikuwa kibaridi sana. Basi nilizamia infoo kwenye zinga
la mnuso huko saiti za upanga. Nilifika getini nikakuta baunsa kanyuti chedro
likisubiri kumtoa noma kila mzamiaji. Alikuwa mnoko kishenzi. Akatema mkwara
mbuzi, nikajibu kwa mkwaradume....akabloo mimi ndani’.
Maana
ya Maneno
1.
Wikiendi – Mwisho wa wiki
2.
Kibaridi –tulivu
3.
Kuzamia infoo – Kuingia mahali bila kualikwa
4.
Zinga la Mnuso –sherehe kubwa
5.
Saiti –sehemu
6.
Baunsa limenyuti chedro – Ni mlinzi wa mlangoni ametulia pembeni
7.
Noma – Hatari
8.
Mnoko kishenzi – kinaa sana
9.
Mkwara mbuzi – Vitisho dhaifu (Sani, Toleo Na 49).
Mtu
asomapo maelezo hayo, mara moja unaona jinsi vijana hawa wa rika moja waishio
mjini wanavyozungumza Kiswahili. Si rahisi kwa mzungumzaji wa Kiswahili sanifu
kuielewa kirahisi lugha hiyo.
Dhima za Rejesta
Katika
kipengele cha utambulisho wa kijamii tunaangalia namna aina ya lugha ya
mazungumzo inavyoweza kujidhihirisha miongoni mwa watumiaji wake au
kuwatambulisha na kuwatofautisha wanajamii husika. Pia katika utambaulisho wa
kijamii tunaangalia vile ambavyo mtu hutambulika katika jamii kulingana na namna
anavyoongea kulingana na hadhi, tabaka, na jinsi ambavyo mtu huyo anavyoweza
kusababisha mshikamano au mwachano katika mazungumzo. Kwa mfano jamii
itamtambua mwanajamii kuwa ni msomi kulingana na mtindo wa lugha ya mazungumzo
anaoutumia, au ni mtu wa mtaani kulingana na lugha anayotumia.
Rejesta,
ina nafasi kubwa sana katika maendeleo ya kiuchumi kwa mtu binafsi na taifa kwa
ujumla. Hii ni kutokana na kwamba, madhumuni makuu ya mawasiliano katika
biashara ni kuwavutia wateja na kuwafanya kuamini kuwa bidhaa ama huduma
wanazouziwa ni za kiwango cha juu na ni thamani bora kwa pesa zao. Hivyo lugha
ya biashara (rejesta), kwa kawaida ni lugha ya kutangaza uzuri wa bidhaa au
huduma, huwa na sentensi au vifungu vifupi, mfano “Okoa mapesa chungu mbovu”
pia huwa na lugha ya kupumbaza na kuaminisha, mfano “Kunywa XYZ kufumba na
kufumbua afya yako itakurudia”.
Pia
rejesta inasaidia sana kurahisisha mawasiliano miongoni mwa wazungumzaji katika
masuala mbalimbali ya kibiashara na hata katika huduma mbalimbali za kijamii.
Mfano hospitalini “mbili mara tatu”, hotelini “kuku wali tafadhali”, sokoni
“kata nusu” na maeneo mengine.
Baadhi
ya rejesta hutumika kupunguza idadi ya maneno hivyo kufanya mazungumzo yawe
mafupi na yanayoeleweka kwa urahisi mfano rejesta za hotelini kama vile:-
Muuzaji: wapi ng’ombe? Mteja: hapa Muuzaji: wapi chai chapati? Mteja: hapa.
Pia
katika kutolea elimu ya dini kanisani na msikitini rejesta ina nafasi kubwa
katika kujenga maadili.
Vilevile
rejesta ina nafasi ya kupamba mazungumzo, wazungumzaji wengi wanapozungumza
hapa na pale hupenda kutumia maneno tofautitofauti ili kufanya mazungumzo yawe
ya kuvutia. Mfano mazungumzo miongoni mwa vijana:
Kijana
1: Niaje? Nakuona umechili
Kijana
2: mzuka jembe. Kama kawa… kama dawa!
MISIMU
Misimu
ni semi za muda na mahali maalum ambazo huzuka na kutoweka kutegemea mazingira
maalum. misimu inayodumu huweza kuingia katika methali, nahau au misemo ya
lugha ya jamii hiyo.
Chanzo cha Misimu
1.
Misimu huzuka kulingana na mabadiliko ya kihistoria yanayoikumba jamii husika
katika nyakati mbalimbali.
2.
Misimu huzuka kutokana na haja ya watu kuelezea hisia zoa juu ya matukio
mbalimbali yaliyotokea katika vipindi fulani kwa mfano, njaa, mafuriko, vita
n.k.
Aina za Misimu
1. Misimu ya pekee. Hii ni misimu ambayo huelezea
mahusiano ya kikundi kimoja kutoka katika utamaduni mmoja, na hujulikana
miongoni mwao pekee.
2. Misimu ya kitarafa. Misimu hii hujulikana na watu wengi
katikia eneo kubwa, yaweza kuwa ni kata, wilaya au tarafa.
3. Misimu zagao. Ni misimu iliyoenea nchi nzima au
pengine kuvuka mipaka ya nchi, misimu hii husikika redioni, magazetini na hata
kwenye vitabu. Msimu uliokita mizizi sana huweza kusanifishwa na kuwa msamiati
rasmi.
Sifa za Misimu
1.
Huzuka na kutoweka kufuatana na mabadiliko ya jamii
2.
Ni lugha isiyo sanifu
3.
Ina chuki
4.
Ni lugha ya mafumbo
5.
Ina maana nyingi
Dhima ya Misimu
1.
Hutumika kupamba lugha
2.
Hutumika kukuza lugha
3.
Hutumika kutunza historia ya jamii fulani
4.
Hutumika kuibua hisia mbalimbali za wazungumzaji
5.
Hufurahisha na kuchekesha
LUGHA YA KIMAZUNGUMZO
NA YA KIMAANDISHI
Sifa ya Lugha ya
Kimazungumzo
Lugha
ya mazugumzo ni maongezi ya watu wawili au zaidi bila kutumia maandishi. Lugha
ya mazungumzo ambayo ndiyo lugha kongwe zaidi ya lugha ya maandishi ina dhima
kubwa ya kufanikisha mawasiliano miongoni mwa watu au kikundi fulani. Lugha hii
ya mazungumzo ilianza punde tu binadamu alipoanza kukabiliana na mazingira
yake, hivyo kimsingi lugha ya mazungumzo ndiyo nguzo kuu ya kufanikisha shughuli
zote za kibinadamu kutokana na nafasi yake kimatumizi.
Faida ya Lugha ya Mazungumzo
1.
Mzungumzaji anaweza kukaa ana kwa ana na msikilizaji, hivyo hukuza uhusiano.
2.
Mzungumzaji anaweza kutumia ishara za mwili katika kusisitiza maelezo yake.
3.
Mzungumzaji anaweza kupata nafasi ya kuuliza au kuulizwa maswali.
4.
Mzungumzaji anaweza kuonesha hisia zake kwa kulia, kupaza sauti, kupunguza
sauti, kuonyesha furaha huzuni au hasira.
5.
Mzungumzaji anaweza kuuliza maswali, kuona hisia za mzungumzaji kwa kusikiliza
lugha zinazotolewa na kuangalia ishara za mwili zinazotumika.
6.
Mzungumzaji anaweza kupata nafasi ya kufuta usemi wake, kuongezea jambo au
kutoa maelezo ya ziada.
7.
Mzungumzaji anaweza kubadilisha lugha yake kulingana na mazingira aliyomo.
8.
Mzungumzaji anao uhuru wa kutumia lugha ya mitaani, misimu kulingana na
muktadha.
Matatizo ya Lugha ya Mazungumzo
1.
Maelezo lazima yahifadhiwe kichwani, hivyo kama mtu hana kumbukumbu, taarifa
zilizotolewa hupotea na kusahaulika.
2.
Mtumiaji wa lugha ya mazungumzo anaweza kurudiarudia vipengele fulani na hivyo
kuichosha hadhira.
3.
Ujumbe unaweza usieleweka kama unatolewa kwenye kelele nyingi
LUGHA YA MAANDISHI
Hii
ni lugha inayowasilishwa kwa njia ya maandishi. Lugha ya maandishi huzihusiha
pande mbili, mwandishi na msomaji. Lugha ya maandishi sharti iwe fasaha ili
msomaji anaposoma maandishi hayo, apate kuelewa kila kitu, yaani asibaki
akijiuliza maswali. Lugha
ya maandishi huambatana na alama za uakifishaaji, hii husaidia maandishi
kusomeka vizuri na kueleweka kwa urahisi
Ubora wa Lugha ya Maandishi
1.
Lugha ya maandishi huwawezesha watu walio mbali kuwasiliana.
2.
Lugha ya maandishi hustawisha sarufi ya lugha na misingi yake, kwa sababu
mwandishi anahakikisha kwamba anazingatia vizuri kanuni za kisarufi ili msomaji
wake aweze kumwelewa.
3.
Ili kuhakikisha maelezo yake yanaeleweka mwandishi analazimika kuandika kwa
uwazi na kwa kuzingatia kanuni na miiko yote ya uandishi.
Udhaifu wa Lugha ya Maandishi
1.
Lugha hii hutumiwa na wale tu wanaojua kusoma na kuandika.
2.
Lugha ya maandishi haina msisimko uletwao na lafudhi na matamshi.
3.
Msomaji hukosa vidokezo vingi ambavyo katika lugha ya mazungumzo huchangia
katika mawasiliano.
4.
Lugha ya maandshi inamnyima mwandishi nafasi ya kupima welewa wa msomaji kwa
kuwa hamwoni.
Dhima ya Lugha ya
Mazungumzo na Lugha ya Maandishi
Lugha
ya mazungumzo na lugha ya maandshi zote zina umuhimu wa pekee katika maisha ya
kila siku kwa sababu ndizo zinzaowezesha watu kuwasiliana kwa namna mbalimbali.
Umuhimu
wa lugha ya maandshi pia hutokana na dhima yake kwa watu. Maandishi yanaweza
kuhifadhiwa na kusambazwa kwa watu wengi hata walio mbali. Maandishi
yanahifadhi kumbukumbu na kwa muda mrefu. Kwa hali hii, watu wa vizazi vingine
wanaweza kusoma na kujua mambo yaliyofanyika karne nyingi zilizopita.
Tofauti kati ya Lugha
ya Mazungumzo na Lugha ya Maandishi
1.
Lugha ya mazungumzo huwezesha mawasiliano ya ana kwa ana lakini lugha ya
maandishi haiwezeshi mawasiliano ya ana kwa ana.
2.
Lugha ya mazungumzo haihitaji maandalizi wakati lugha ya maandishi huhitaji
maandalizi. Mwandishi atalazimika kupata muda wa kuandika pamoja na kuandaa
vifaa kama vile kalamu, karatasi n.k
3.
Lugha ya mazungumzo hailazimiki kuzingatia kanuni za kisarufi, lakini lugha ya
maandshi hutakiwa kuzingatia kanuni za kisarufi.
Tofauti nyingine kati ya lugha ya
maandishi na lugha ya mazungumzo huweza kuonyeshwa katika jedwali lifuatalo:
Kipengele
|
Mazungumzo
|
Maandishi
|
Muktadha
|
|
|
Mada
|
Hazina
uzito mkubwa
|
Huelekea
kuwa na uzito mkubwa.
|
Mpangilio wa mada na mawazo
|
Hautabiriki.
Unaelekea kutokuwa na mtiririko.
|
Hutabirika.
Huelekea kuwa na mtiririko.
|
Mjadala wa mada
|
Hauelekei
kuwa na kina. Hazichujwi kwa uaangalifu.
|
Unaelekea
kuwa na kina. Huchujwa.
|
DHIMA YA MATUMIZI YA
LUGHA
Dhima
kuu ya lugha ni kupashana habari, ujuzi na maarifa mbalimbali. Vilevile lugha
husaidia kujenga uhusiano mwema baina ya watu. Uhusiano huo unaweza kuwa wa
kijamii, kielimu, kibiashara, kihuduma, kisiasa, kiuchumi n.k. Kwa hiyo, kujua
jinsi ya kuitumia lugha kama inavyotakiwa, kunasaidia kufikisha vizuri ujumbe
unaotakiwa bila kuupotosha. Vilevile kunasaidia kuepuka migongano, hasa ya
kijamii kwa kuwa utakuwa umetumia lugha kwa mujibu wa mila na desturi za jamii
inayohusika.
Mambo ya Kuzingatia
katika Matumizi ya Lugha
1. Mada
inayozungumziwa: Mada
za mazungumzo zipo nyingi. Kuna mada za kijamii, kwa mafano ndoa, unyago,
mapenzi, kifo, matanga, burudani, muziki n.k. Kuna mada za kibiashara kwa mfano
bidhaa, kodi, vibali, fedha, hasara, faida n.k. Kwa hiyo, ili mazungumzo yaweze
kwenda vizuri, wazungumzaji wanatakiwa kuzingatia mada husika.
2. Muktadha wa
mazungumzo: Mazungumzo
yanaweza kuathiriwa na miktadha tofauti. Kwa mfano kuna miktadha ya kidini,
kiganga, huzuni, sherehe, kisiasa, kielimu, kibiashara n.k. Mazungumzo yanaweza
kufanyika mjini, kijijini, ugenini, shuleni, dukani, hotelini n.k
3. Malengo ya
mazungumzo hayo: Malengo
ya mazungumzo nayo yanaathiri matumizi ya lugha. Kwa mfano, lengo linaweza
kutoa taarifa, kuhoji, kukejeli, kutia moyo n.k. Sasa jinsi lugha
itakavyotumika katika kutoa taarifa ni tofauti na itakavyotumika katika kutia
moyo au kukejeli.
4. Uhusiano uliopo
baina ya wazungumzaji: Matumizi ya lugha huweza kuathiriwa pia na mahusiano ya
wazungumzaji. Kuna mazungumzo baina ya watoto, wanafunzi, wazee, viongozi,
marafiki n.k. Upo uhusiano wa daktari na mgonjwa, mwalimu na mwanafunzi,
mnunuzi na muuzaji. Kwa hiyo mazingira baina ya pande hizi mbili yatategemea
uhusiano wao, kwa hiyo kaida za uhusiano huu utapaswa kuzingatiwa. Kwa hiyo,
kwa kuzingatia mambo haya manne, itawafanya wazungumzaji wawe makini katika
uteuzi wa maneno, miundo, mifano na kina cha ufafanuzi wa maelezo au habari
inayozungumzwa.
Dhima ya Lugha ya
Kimazungumzo na ya Kimaandishi
Lugha
ya kimazungumzo na ya kimaandishi zina dhima kuu ya kupasha habari, ujuzi, na
maarifa mbalimbali, husaidia kujenga uhusiano mwema baina ya watu, kufikisha
ujumbe unaotakiwa vizuri bila kupotosha, kufundishia ujuzi, kuchochea
maendeleo, kuhifadhi historia ya jamii na kueleza mawazo au hisia za watu.
Lugha ya Kimazungumzo
na ya Kimaandishi katika Miktadha Sahihi
Matumizi
ya lugha ya kimazungumzo na ya kimaandishi katika muktadha sahihi huongozwa na
mambo yafuatayo, ambayo ni mada inayozungumzwa, muktadha au mahali mazungumzo
hayo yanapofanyika, malengo ya mazungumzo hayo na uhusiano uliopo kati ya
wazungumzaji.
Zoezi 1
Tumia
lugha ya kimazungumzo na ya kimaandishi katika miktadha sahihi.
MATAMSHI NA LAFUDHI YA
KISWAHILI
Matamshi
ni namna ambavyo mtu anatamka neno au jinsi mtu anavyozungumza lugha. Unaposema
fulani ana matamshi mazuri ya Kiswahili utakuwa unamaanisha anazungumza
Kiswahili fasaha.
Neno
moja linaweza kuzungumzwa/kutamkwa kwa namna tofauti na watu mbalimbali
kutokana na sababu mbali mbali, sababu hizo ni pamoja na eneo la kijiografia
anakotoka huyo mtu, kabila lake, kundi lake la kijamii mfano msanii au
mwanasiasa, na elimu aliyonayo. Hizi zote zinaweza zikawa ni sababu za kufanya
watu watofautiane katika matamshi.
Lafudhi Mbalimbali za
Kiswahili
1.
Sauti za lugha husika
2.
Mkazo
3.
Kiimbo
SAUTI ZA LUGHA YA
KISWAHILI
Sauti
za lugha ya Kiswahili hujumuisha irabu na konsonanti, ambazo kwa ujumla huunda
sauti 24, irabu tano na konsonanti 19 (konsonanti x na q hazipo katika matamshi
ya kiswahili). Sauti za Kiswahili hutamkwa kama zilivyoandikwa, kwa mfano
maneno “data” au “dengue” wewe unayatamkaje? Wengi huyatamka kama yalivyo hata
kama wakiwa wanazungumza kiingereza, hii ni kwa sababu maneno ya Kiswahili
hutamkwa kama yalivyoandikwa.
Kwa
hiyo unapotamka maneno ya Kiswahili ni sharti uzingatie sauti asilia za lugha
ya Kiswahili. Kuna watu huwa wanaandika hivi “xaxa”, hii huwa unaitamkaje? Au
“ucjal” huwa unaitamkaje? Kwa kufuata matamshi asilia ya Kiswahili “ucjal”
itatamkwa “uchijal” sijui itakuwa ina maana gani sasa. Na pengine umekuwa
ukitumia maandishi ya namna hii hata kwenye insha zako ukidhani upo sahihi au
ni kwa mazoea tu, sasa kwa kuwa umejua matamshi sahihi ya Kiswahili ni yapi,
utajifunza kuyatumia kwa usahihi katika maandishi rasmi na yasiyo rasmi.
MKAZO
Katika
lugha ya Kiswahili kuna namna ya kutamka maneno ili kuleta maana mbali mbali,
kwa mfano neno “barabara” litaleta maana husika kulingana na jinsi
lilivyotamkwa. Hivyo, mkazo ni pale silabi inapotamkwa kwa kukazwa. Maneno ya
Kiswahili huwa na silabi moja ambayo hutamkwa kwa nguvu zaidi kuliko silabi
nyingine. Unapotamka silabi iliyotiwa mkazo, sauti hupandishwa juu kiasi.
Maneno
mengi ya Kiswahili, hasa yale yenye asili ya Kibantu hutia mkazo katika silabi
ya pili kutoka mwisho.
Kwa
mfano:ba’bu, maya’i, rama’ni (mimi nilikuwa nikitamka ra’mani), baraba'ra
(njia).
Baadhi
ya maneno yenye asili ya kigeni, huwa na mkazo katika silabi nyingine. Kwa
mfano: bara'bara (sawa sawa), Alha’misi
KIIMBO
Ni
utaratibu maalum wa upandaji na ushukaji wa mawimbi ya sauti unaojitokeza
katika utamkaji wa lugha fulani.
Katika
utaratibu wa utamkaji, dhana ya Kiimbo huandamana pia na dhanna ya kidatu
( yaani kiwango cha juu, cha chini au cha kati cha sauti katika usemaj),
Kwa hivyo ni muhimu hapa kueleza tofauti zilizopo baina ya kiimbo na kidatu.
Wakati kiimbo kina maana ya kupanda na kushuka kwa mawimbi ya sauti ya lugha,
kidatu kina maana ya kiwango cha sauti isikikayo, wakati wa utamkaji ama kuwa
juu, kuwa katikati au kuwa chini.
Aina za Viimbo
1. Kiimbo cha maelezo:
Kiimbo
cha maelezo ni kile ambacho kwa kawaida msemaji wa lugha akiwa kwenye kidatu
chochote kile mawimbi sauti ya usemaji wake yanakuwa takriban katika
mstari ulionyooka. Mfano, Mwalimu anafundisha.
2. Kiimbo cha maulizo:
Kiimbo
cha kuuliza hujitokeza kwa kutumia viwango tofauti vya kidatu kutegemeana na
aina ya swali linaloulizwa. Mfano, mwalimu anafundisha?
3. Kiimbo cha amri:
kiimbo
cha amri hakitofautiyani sana na kiimbo cha maulizo. Kiimbo cha amri,
mzungumzaji hutumia kidatu cha juu zaidi kuliko ilivyo katika kiimbo cha
maelezo. Mfano, njoo hapa!
LAFUDHI YA KISWAHILI
Lafudhi
ni matamshi ya msemaji wa lugha fulani ambayo yanatokana na athari za
kimazingira. Mazingira hayo yanaweza kuwa eneo atokalo mtu, mahali alikosomea,
kiwango chake cha elimu, tabaka lake la kijamii na kadhalika.
Lugha
ya Kiswahili ni lugha ya pili kwa watumiaji wengi wa afrika mashariki, kwa hiyo
hii inafanya kuwatambua wazungumzaji wa Kiswahili kulingana na makabila yao au
maeneo wanakotoka. Kwa mfano, kwa hapa Tanzania tunaweza kuwatambua watu wa
mwanza kwa lafudhi yao, watu wa mtwara kwa lafudhi yao, watu wa pemba kwa
lafudhi yao au watu wa Musoma kwa lafudhi yao.
Mifano
1.
Usiniretee maswara ya ubaguzi wa kikabira hapa (Wakuria)
2.
Amemupiga mutoto ya watu juu amemuibia mfaranga makumi mawili (Wakongo)
3.
Ukikaa nchale, ukichimama nchale (Wamakonde)
4.
Wewe unakamuaga mang’ombe tu moja kwa moja (Wasukuma)
5.
Mbona unakuwa kinganganizi, nilishakwambia sikupendi lakini wewe bado
unaningangania tu! (Wahaya)
UTATA KATIKA MAWASILIANO
Utata
ni hali ya neno au sentensi kuwa na maana zaidi ya moja. Kwa hiyo tungo tata ni
tungo ambayo inaweza kuwa na maana zaidi ya moja.
Sababu za Utata
Utata
katika tungo hutokea kwa sababu zifuatazo:
1.
Neno kuwa na maana zaidi ya moja, kwa mfano neno mbuzi,
kata n.k.
2.
Kutozingatia taratibu za uandishi, Mfano; Tulimkuta Nyammy na rafiki yake,
Mazala vs Tulimkuta Nyammy na rafiki yake Mazala. Katika
sentensi hizi alama (,) ndio huleta tofauti, sentensi ya kwanza inamaana
kulikuwa na watu wawili Nyammy na rafiki yake aitwaye Mazala na sentensi ya
pili isiyo na alama (,) inamaanisha kulikuwa na watu wawili Nyammy na mtu
mwingine ambaye ni rafiki yake Mazala
3.
Kutumia maneno bila kuzingatia muktadha wa matumizi ya maneno hayo.
4.
Utamkaji wa maneno. Wakati mwingine utata unaweza kujitokeza katika matamshi
tu, ili hali katika maandishi utata hauonekani. Kwa mfano; Mimina wewe, katika
maandishi linaweza kuandikwa mimi na wewe, na hivyo kuondoa utata.
5.
Mjengo wa maneno. Utata huu huzuka katika vitenzi kama pigia. Chanzo cha
utata katika kitenzi hiki ni kiambishi –i-. Kiambishi hiki
kinaweza kumaanisha: kwa ajili ya…, kwa sababu ya.., kwa kutumia chombo
fulani.., au mahali fulani.
Mfano:
1.
Alimpigia ukorofi wake (kwa sababu ya)
2.
Alimpigia kiatu (kifaa)
3.
Alimpigia ndani (mahali)
Mifano ya utata katika
tungo
1. Patience
amemwandikia Lilian barua: Sentensi hii huweza kuwa na maana
kuwa Patience ameandika barua kwenda kwa Lilian au Patience ameandika barua kwa
niaba ya Lilian
2. Umefanikiwa
kununua mbuzi? Sentensi
hii huweza kumaanisha ununuzi wa mbuzi mnyama au mbuzi kifaa cha kukunia nazi.
3. Alimkuta amelala
kwenye nyumba ya wageni: Sentensi hii huweza kumaanisha,
nyumba ya mtu lakini inatumika kwa ajili ya wageni kwa malipo au ni nyumba
inayomilikiwa na watu ambao ni wageni katika eneo lile.
4. Attu ametumwa na
Aritamba: Sentensi
hii inaweza kueleweka kumaanisha, Aritamba amemtuma Attu au Attu na Aritamba
wametumwa wote kwa pamoja
Thank you so much, but is their a way that we can download this notes?
ReplyDeleteBut please keep up the good work