Join Our Groups
TOPIC 7: USIMULIAJI WA MATUKIO
Njia za Usimulizi wa
Matukio
Usimulizi
hufanyika kwa njia kuu mbili yaani kwa njia ya maandishi na kwa njia ya
masimulizi ya mdomo. Kila njia hutegemea kwa namna msimuliaji anavyoweza
kuwasiliana na msikilizaji. Ikiwa msimuliaji na msikilizaji hawakukaribiana,
njia ambayo itatumika ni ile ya maandishi. Kwa mfano kama utahitaji kumweleza
mtu aliyembali kuhusu tukio fulani la kusisimua utalazimika kutumia maandishi,
yaani utatumia njia ya kumwandikia barua.
Lakini
kama unamsimulia mtu ambaye yupo karibu nawe, utatumia njia ya mazungumzo ya
ana kwa ana.
Taratibu za Usimulizi
wa Matukio
Usimulizi
wa matukio dhamira yake ni kumweleza mtu au watu tukio ambalo wao
hawakulishuhudia. Hivyo katika usimulizi msimuliaji hutakiwa kutoa maelezo
muhimu ambayo yatawawezesha watu hao kulielewa tukio linalosimuliwa sawasawa na
huyo anayeshuhudia.
Mambo
muhimu ya kutaja katika usimulizi wa matukio ni pamoja na haya yafuatayo:
1. Aina ya tukio – msimuliaji atatakiwa kubainisha
katika maelezo yake aina ya tukio. Kwa mfano, kama ni harusi, ubatizo, ajali ya
barabarani au mkutano.
2. Mahali pa tukio – ili msimuliaji aweze kuielewa
habari inayosimuliwa, ni lazima kumwelewesha ni mahali gani tukio hilo
limetokea. Kwa mfano, kama ni mjini inafaa kutaja hata jina la mtaa.
3. Wakati – katika usimulizi ni muhimu pia
kutaja muda ambao tukio limetendeka kama ni asubuhi, mchana au jioni bila
kusahau kutaja muda halisi yaani ilikuwa saa ngapi.
4. Wahusika wa tukio – ni muhimu kutaja tukio limehusisha
watu gani, wingi wao, jinsia yao, umri wao n.k.
5. Chanzo cha tukio – kila tukio lina chanzo chake hivyo
ni muhimu kutajwa katika usimulizi.
6. Athari za tukio – athari za tukio nazo ni sharti
zibainishwe. Kama ni ajali, je watu wangapi wameumia; wangapi wamepoteza maisha
n.k.
7. Hatima ya tukio – msimuliaji katika usimulizi wake
ni lazima abainishe baada ya tukio kutokea na kushughulikiwa hatima yake
ilikuwaje. Kwa mfano, kama tukio ni ajali ya barabarani hatima yake inaweza
kuwa majeruhi kupelekwa hospitalini na dereva aliyehusika kukamatwa.
Kwa
hiyo misingi hii ya usimulizi hufanya usimulizi wa tukio kuwa na sehemu kuu
tatu:
1. Utangulizi – sehemu hii huwa na maelezo tu ya
utangulizi ambayo hulenga kuvuta hisia na umakini wa msikilizaji au
wasikilizaji. Kwa kawaida utangulizi wa tukio huwa ni maneno machache kiasi
yasiyozodi aya moja.
2. Kiini – kiini cha usimulizi huelezea tukio
halisi kuanzia chanzo chake, wahusika, muda, mahali na athari za tukio.
3. Mwisho – mwisho wa usimulizi ni matokeo yanayoonyesha
matokeo ya mwisho ya tukio linalohusika, wakati mwingine matukio haya yanaweza
kuambatana na maelezo ya msimuliaji kuhusu mtazamo au maoni yake binafsi juu ya
tukio ambalo amesimulia.
Mbinu za Usimulizi
Ili
habari inayosimuliwa ipate kueleweka vizuri, sharti msimuliaji ajue mbinu za
kusimulia katika hali inayovuta hisia za msikilizaji wake. Baadhi ya mbinu hizo
ni uigizi, utumizi wa lugha fasaha inayozingatia lafudhi sahihi ya Kiswahili. Kwa
upande wa uigizi msimuliaji atatakiwa kuigiza mambo muhimu yanayohusiana na
tukio ambalo anasimulia. Nayo ni kama vile milio, sauti na matendo.
EmoticonEmoticon