Join Our Groups
TOPIC 1: MAWASILIANO
Katika mada hii unatarajiwa kuelewa fasili ya mawasiliano na jinsi mchakato wa mawasiliano unavyofanyika. Utaelewa dhana ya lugha na vipengele muhimu vinavyokamilisha fasili ya lugha. Utaelewa dhima kuu za lugha, matumizi na umuhimu wake. Vilevile katika mada hii utajifunza juu ya lafudhi na matamshi mbalimbali ya watumiaji wa lugha ya Kiswahili.
Lugha kama
Chombo cha Mawasiliano
Mawasiliano
ni mchakato wa kuhawilisha taarifa kwa njia ya ubadilishanaji wa mawazo, hisia,
malengo, tabia, matarajio, mitazamo kupitia mazungumzo, ishara na maandishi. Ni
ubadilishanaji wa taarifa unaoleta maana baina ya pande mbili au zaidi ambazo
zinaweza kuwa viumbe hai au kinyume chake. Sasa hapa sisi tutajikita katika
mawasiliano yanayofanywa baina ya viumbe wanaotumia lugha (ambao kimsingi ni
binadamu).
Maana ya
Mawasiliano
Lugha
ni nyenzo muhimu sana katika mawasiliano ya binadamu. Ulishawahi kujiuliza
kwamba mwasiliano yangekuwaje pasipokuwepo lugha? Mwalimu angekua anatumia
mtindo gani kukufundisha darasani au wewe ungemwombaje kalamu rafiki yako?
(Unasema ungewasiliana kama wanavyowsiliana watu wasiosikia au kuzungumza?) Hao
pia wanawasiliana hivyo kwa sababu wana maarifa ya lugha.
Mafumbuzi
ya kisayansi na teknolojia, yote haya yasingewezekana pasipo kutumia lugha,
usingeweza kusogoa (kuchat) na marafiki zako kwenye facebook, usingeweza
kumwandikia ujumbe rafiki yako kupitia simu yako na kadhalika.
Umeona
sasa jinsi lugha ilivyo muhimu katika mwasiliano? Kabla hatujaona umuhimu huu
hebu tuangalie fasili/maana ya lugha.
Kuna
mitazamo mbalimbali juu ya fasili ya lugha lakini kwa ujumla lugha inaweza
kufasiliwa kama mfumo wa sauti za nasibu zilizokubaliwa na watu au jamii ili
zitumike katika mawasiliano yao ya kila siku ili kuelezea hisia, mawazo,
matakwa na mahitaji yao.
Kulingana
na fasili hii tunaweza kubainisha maneno ya msingi yanayojitokeza katika fasili
ya lugha, maneno hayo ni pamoja na haya yafuatayo:
Lugha ni Mfumo
Kila
lugha ya mwanadamu imeundwa katika mifumo miwili mikuu; mfumo wa sauti na mfumo
wa maana. Lugha huundwa kwa sauti ambazo huunganishwa kuunda neno au sehemu ya
neno, maneno nayo huungana kuunda miundo mikubwa zaidi yenye maana kama virai,
vishazi, sentensi na aya.
Mfano;
k+u+k+u – kuku
Mtoto
+ anatembea – mtoto anatembea
Katika
muunganiko huu wa maneno na miundo mbali mbali, huwa kuna kanuni na sheria
zinazodhibiti mfuatano wa kila kipashio. Kuna kanuni zinazodhibiti mfuatano wa
sauti, mfuatano wa mofimu, mfuatano wa maneno na hata mfuatano wa sentensi. Kwa
maana hiyo, lugha ya mwanadamu ni mfumo wenye kanuni, sheria na taratibu
maalumu ambazo zikikiukwa basi kunakuwa hakuna utimilifu wa lugha husika.
Sheria hizi zinazotawala mpangilio wa viunzi vya lugha hiyo ndizo
zinazowawezesha watumiaji wa lugha fulani kuelewana.
Lugha ni Mfumo
wa Sauti Nasibu
Lugha
ni ya nasibu kwa maana kwamba, hakuna uhusiano wa moja kwa moja kati ya neno
(kwa mfano jiwe) na kitu chenyewe tunachotumia katika ujenzi na matumizi
mengine (maana na kirejelewa). Hii ina maana kwamba, maumbo ya ishara za kiisimu
hayana uhusiano wowote au mfanano wowote na maana ambazo tunayapa. Kwa mfano
neno “jiwe” hakuna watu waliokaa na kusema kuanzia leo hili litaitwa jiwe. Vile
vile hakuna uhusiano wowote kati ya neno “jiwe” na umbo linalorejelewa.
Uhusiano wake ni wa nasibu tu na hutofautiana kutokana na lugha moja na
nyingine. Jiwe mnaliitaje katika lugha yenu? Basi huo ndio unasibu wa lugha.
Lugha ni Maalumu
kwa Mwanadamu
Lugha
ni chombo cha mawasiliano ambacho amejaliwa binadamu tu na kwamba hakuna kiumbe
mwingine ambaye si binadamu mwenye uwezo wa kuzungumza na kutumia lugha. Hii
ina maana kuwa kuna sifa fulani za lugha za binadamu ambazo hazipatikani kwa
kiumbe mwingine yeyote yule isipokuwa mwanadamu. Ingawa ndege, mbwa, nyuki,
tumbili wanaweza kuwasiliana, mawasiliano yao huwa ni ya sauti au ishara ambazo
kimsingi siyo lugha, pia huwa yanadhibitiwa na hisia tu kama hofu, njaa, na
ishara za kutoa taarifa. Binadamu ana uwezo wa kujifunza lugha mbalimbali na
kuitumia katika mazingira yake na kitu ambacho wanyama hawawezi. Kwa mfano,
ukimchukua paka wa china na kumleta Tanzania atatoa sauti ile ile sawa na paka
wa Tanzania kwa kueleza shida ile ile au kutoa ishara ile ile.
Lugha ni Mfumo
wa Ishara
Uishara
wa lugha unamaanisha kuwa maneno huambatanishwa/huhusishwa na vitu,
matendo,mawazo au hisia kwa makubaliano ya unasibu tu. Vile vile, yale
tunayoyasoma katika maandishi ni ishara tu, maana zake lazima zipatikane katika
muktadha wa mawasiliano. Hivyo basi, tunapojifunza lugha lazima tufahamu mfumo
wa alama za lugha hiyo na kuelewa uhusiano uliopo kati ya ishara na vitu
vinavyowakilishwa.
Lugha Hutumia
Sauti
Sifa
kuu ya lugha ni kutumia sauti ambazo hutengenezwa na ala za sauti. Pamoja na
maendeleo ambayo mwanadamu ameyafikia kwa sasa katika uandishi na uwasilishaji
wa taarifa kwa kutumia lugha sauti ndiyo msingi wa kila kitu. Hii ni kutokana
na ukweli kwamba:
Mtoto
hujifunza kuzungumza kabla hajajifunza kusoma na kuandika.
Mtoto
hujifunza lugha moja kwa moja bila kufikiri kadiri anavyokuwa
Maandishi
yalikuja baada ya mazungumzo
Maandishi
huwasilisha yale yanayozungumzwa
Watu
kwa kawaida hutumia muda mwingi kuzungumza kuliko kuandika
Kuna
mambo mengi ya muhimu katika sauti za lugha ambayo hayawezi kuwasilishwa vema
kwa kutumia maandishi. Mambo hayo ni kama, kiimbo, toni, mkazo, kidatu; haya ni
muhimu katika mawasiliano lakini hayawezi kuwasilishwa kisawasawa kwa kutumia
maandishi
Lugha ni kwa ajili ya Mawasiliano
Kwa
kutumia lugha binadamu anaweza kufanya vitu ambavyo viumbe wengine hawawezi
kuvifanya. Vile vile lugha hutuwezesha sisi kuzungumzia hisia zetu, matamanio
yetu, kucheza, kufanya kazi n.k. Yote haya yanawezekana kwakuwa tunayo lugha
ambayo ndiyo nyenzo kuu ya mawasiliano.
Mfumo wa Lugha
Hoja
kuwa lugha ni mfumo inamaanisha kuwa lugha ina muundo unaohusisha viambajengo
mbalimbali. Viambajengo au vipashio hivi ni sauti, neno na sentensi. Kwa
pamoja, vipashio hivi hushirikiana kuunda tungo zenye maana na kama tungo hizo
hazina maana au kama haziwasilishi ujumbe wowote basi tunasema haziwi lugha.
DHIMA ZA LUGHA
KATIKA MAWASILIANO
Baadhi ya dhima
za lugha ni pamoja na hizi zifuatazo:
Ujumi:
ujumi ni hali ya kutumia maneno ya lugha fulani kwa ufundi na ustadi wa hali ya
juu kwa lengo la kuburudisha na kuwavutia watu wengine. Baadhi ya watu hutumia
lugha kwa dhima hiyo, ili maksudi wasomaji au wasikilizaji wao wavutike na
kuburudishwa na Lugha hiyo. Maeneo yatumikamo lugha yenye ujumi wa kiwango cha
juu ni kwenye matangazo na kwenye fani ya utunzi wa mashairi.
Utambuzi:
Ni hali ya kufikiria kwa makini, kukokotoa na kutoa majibu ya maswali tofauti
ndani ya ubongo. Chombo kikuu kitumikacho kutoa majibu hayo ni lugha. Kutokana
na muktadha huo tunaweza kusema kwamba lugha hutumika kama chombo cha utambuzi.
Hisia:
ni fikra za ndani alizokuwa nazo kiumbe mwanaadamu. Tunapotaka kuonyesha hisia
zetu na vilevile kuwavuta wengine kwa maneno mazito yanayoweza kumtoa
msikilizaji machozi ya huzuni au ya furaha tunachagua maneno makali yenye
hisia.
Kujielezea:
Hali ya mtu kudhihirisha mambo mbalimbali aliyokuwa nayo ndani ya moyo wake.
Kwa mfano mtu anaposema nina furaha sana. Hapa mtu anatowa msisitizo wa
kuonyesha kiwango cha furaha alichonacho, hili linafanyika kwa kutumia lugha.
kwa ufupi tunachoweza kusema hapa ni kwamba lugha hutumika kwa ajili ya
kujielezea.
Kuamuru:
Ni kutoa maelekezo kwa njia ya kuamrisha. Kwa mfano hakimu anamuhukumu
mshitakiwa kwa kumuamuru ‘Ninakufunga miaka mitatu jela’. Hapa lugha inatenda
kazi ya kuamuru.
Kushirikiana:
ni hali ya kutenda kitu kwa pamoja au hali ya kuwa na ubiya kwenye jambo. Lugha
huwezesha watu kujenga mahusiano ya siri baina ya watu wawili au zaidi na
kuweza kujitengenezea njia zao za kuwasiliana pasipo wengine kuelewa.
Kuonesha:
kumuelekeza mtu kitu kwa njia ya kuashiria. Unapotaka kuonesha jambo ni lazima
utumiye lugha kwa njia moja au nyengine.
Matumizi na
Umuhimu wa Lugha
Lugha
hutumika kama chombo, zana, kifaa au njia ya kufikia lengo fulani. Baadhi ya
matumizi ya lugha ni pamoja na haya yafuatayo:
1.
Kuwasiliana - Lugha hutumika kupashana habari
2.
Kuunganisha - Lugha hupatanisha na kuleta uelewano miongoni mwa wanajamii. pia
lugha huweza kutofautisha jamii moja na nyengine.
3.
Kujenga jamii - lugha huleta/huhimiza shughuli za maendeleo ya jamii, huleta
amani na mshikamano katika jamii.
4.
Kufundishia - Lugha hutumika katika kufundishia elimu.
5.
Kutambulisha - Lugha hutumika kutambulisha jamii ya watu fulani.
6.
Kuhifadhi - Lugha ndicho chombo cha kuhifadhi na kueneza utamaduni
MATAMSHI NA
LAFUDHI YA KISWAHILI
Matamshi
ni namna ambavyo mtu anatamka neno au jinsi mtu anavyozungumza lugha. Unaposema
fulani ana matamshi mazuri ya Kiswahili utakuwa unamaanisha anazungumza
Kiswahili fasaha.
Neno
moja linaweza kuzungumzwa/kutamkwa kwa namna tofauti na watu mbalimbali
kutokana na sababu mbali mbali, sababu hizo ni pamoja na eneo la kijiografia
anakotoka huyo mtu, kabila lake, kundi lake la kijamii mfano msanii au
mwanasiasa, na elimu aliyonayo. Hizi zote zinaweza zikawa ni sababu za kufanya
watu watofautiane katika matamshi.
Dhana ya matamshi huhusisha:
Sauti za lugha husika
Mkazo
Kiimbo
1.
Sauti za
Lugha ya Kiswahili
Sauti
za lugha ya Kiswahili hujumuisha irabu na konsonanti, ambazo kwa ujumla huunda
sauti 24, irabu tano na konsonanti 19 (konsonanti x na q hazipo katika matamshi
ya kiswahili). Sauti za Kiswahili hutamkwa kama zilivyoandikwa, kwa mfano
maneno “data” au “dengue” wewe unayatamkaje? Wengi huyatamka kama yalivyo hata
kama wakiwa wanazungumza kiingereza, hii ni kwa sababu maneno ya Kiswahili
hutamkwa kama yalivyoandikwa.
Kwa
hiyo unapotamka maneno ya Kiswahili ni sharti uzingatie sauti asilia za lugha
ya Kiswahili. Kuna watu huwa wanaandika hivi “xaxa”, hii huwa unaitamkaje? Au
“ucjal” huwa unaitamkaje? Kwa kufuata matamshi asilia ya Kiswahili “ucjal”
itatamkwa “uchijal” sijui itakuwa ina maana gani sasa. Na pengine umekuwa
ukitumia maandishi ya namna hii hata kwenye insha zako ukidhani upo sahihi au
ni kwa mazoea tu, sasa kwa kuwa umejua matamshi sahihi ya Kiswahili ni yapi,
utajifunza kuyatumia kwa usahihi katika maandishi rasmi na yasiyo rasmi.
2.
Mkazo
Katika
lugha ya Kiswahili kuna namna ya kutamka maneno ili kuleta maana mbali mbali,
kwa mfano neno “barabara” litaleta maana husika kulingana na jinsi
lilivyotamkwa. Hivyo, mkazo ni pale silabi inapotamkwa kwa kukazwa. Maneno ya
Kiswahili huwa na silabi moja ambayo hutamkwa kwa nguvu zaidi kuliko silabi
nyingine. Unapotamka silabi iliyotiwa mkazo, sauti hupandishwa juu kiasi.
Maneno
mengi ya Kiswahili, hasa yale yenye asili ya Kibantu hutia mkazo katika silabi
ya pili kutoka mwisho.
Kwa
mfano:
ba’bu, maya’i, rama’ni (mimi nilikuwa nikitamka ra’mani), baraba'ra
(njia).Baadhi ya maneno yenye asili ya kigeni, huwa na mkazo katika silabi
nyingine. Kwa mfano: bara'bara (sawa sawa), Alha’misi
3.
Kiimbo
Ni
utaratibu maalum wa upandaji na ushukaji wa mawimbi ya sauti unaojitokeza
katika utamkaji wa lugha fulani. Katika
utaratibu wa utamkaji, dhana ya Kiimbo huandamana pia na dhanna ya kidatu (yaani, kiwango cha juu, cha chini au cha kati cha sauti katika usemaj), Kwa
hivyo ni muhimu hapa kueleza tofauti zilizopo baina ya kiimbo na kidatu. Wakati
kiimbo kina maana ya kupanda na kushuka kwa mawimbi ya sauti ya lugha, kidatu
kina maana ya kiwango cha sauti isikikayo, wakati wa utamkaji ama kuwa juu,
kuwa katikati au kuwa chini.
Aina za Viimbo
1.
Kiimbo cha maelezo: Kiimbo cha maelezo ni kile ambacho kwa kawaida
msemaji wa lugha akiwa kwenye kidatu chochote kile mawimbi sauti ya usemaji
wake yanakuwa takriban katika mstari ulionyooka. Mfano, Mwalimu anafundisha.
2.
Kiimbo cha maulizo: Kiimbo cha kuuliza hujitokeza kwa kutumia viwango
tofauti vya kidatu kutegemeana na aina ya swali linaloulizwa. Mfano, mwalimu
anafundisha?
3.
Kiimbo cha amri: kiimbo cha amri hakitofautiani sana na kiimbo cha
maulizo. Kiimbo cha amri, mzungumzaji hutumia kidatu cha juu zaidi kuliko
ilivyo katika kiimbo cha maelezo. Mfano, njoo hapa!
Lafudhi ya
Kiswahili
Lafudhi
ni matamshi ya msemaji wa lugha fulani ambayo yanatokana na athari za
kimazingira. Mazingira hayo yanaweza kuwa eneo atokalo mtu, mahali alikosomea,
kiwango chake cha elimu, tabaka lake la kijamii na kadhalika.
Lugha
ya Kiswahili ni lugha ya pili kwa watumiaji wengi wa Afrika Mashariki, kwa hiyo
hii inafanya kuwatambua wazungumzaji wa Kiswahili kulingana na makabila yao au
maeneo wanakotoka. Kwa mfano, kwa hapa Tanzania tunaweza kuwatambua watu wa
Mwanza kwa lafudhi yao, watu wa Mtwara kwa lafudhi yao, watu wa Pemba kwa
lafudhi yao au watu wa Musoma kwa lafudhi yao.
Mifano:
1.
Usiniretee maswara ya ubaguzi wa kikabira hapa (Wakuria)
2.
Amemupiga mutoto ya watu juu amemuibia mafaranga makumi mawili (Wakongo)
3.
Ukikaa nchale, ukichimama nchale (Wamakonde)
4.
Wewe unakamuaga mang’ombe tu moja kwa moja (Wasukuma)
5.
Mbona unakuwa kinganganizi, nilishakwambia sikupendi lakini wewe bado
unaningangania tu! (Wahaya)
good and educative ilove this site 👍👍👍👍
返信削除Explanation is needed
返信削除